13 November 2013

BODI YA LIGI YAIKAMUA MBEYA CITYNeema Ndugulile
  Timu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga.

  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema pia Mbeya City wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu, baada ya mashabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga, baada ya gharama hizo kuthibitishwa na bodi hiyo.
  "Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mashabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons, baada ya mechi dhidi yao na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitishwa na Bodi ya Ligi," alisema Wambura.
  Alisema Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za mashabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi, Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwani, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.
  Wambura alisema beki wa Coastal Union, Hamad Khamis amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. "Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
  "Nayo Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za mashabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar," alisema Wambura.
  Alisema adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage, ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili.

No comments:

Post a Comment