13 November 2013

KOCHA MPYA AZAM FC KUTUA MAPEMANa Fatuma Rashid
  Kocha mpya wa timu ya Azam Fc anatarajiwa kutua katika kikosi hicho mapema, kabla ya wachezaji wa timu hiyo kurudi kambini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Msemaji wa timu hiyo, Jaffer Iddi alisema wachezaji wote wamepewa likizo ya wiki mbili, hivyo uongozi upo katika mchakato wa kutafuta kocha atakayerithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mwingereza Stewart John Hall.
Msemaji huyo alisema kocha mpya atakapowasili, ndipo atakapojua ni mchezaji gani atataka aanze naye na yupi amalize naye, kwani yeye ndiye atakuwa akiufahamu uwezo wa wachezaji kuanzia mazoezini hadi katika mechi.
Akizungumzia katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, Iddi alisema ilikuwa nzuri kuliko nyingine kwani wote walikuwa wazuri na walipigana kutafuta nafasi nzuri katika kumalizia mzunguko huo.
  Alisema timu yake kwa sasa ipo mapumziko na itarudi kambini baada ya wiki mbili, ili kujipanga zaidi kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo na michuano ya kimataifa.
  Aliongeza kuwa, katika mzunguko wa pili anaimani timu yake itakuwa vizuri zaidi kutokana na kuona pamoja na kupima uwezo wa kila timu shiriki za Ligi Kuu, ambazo uwezo wake wameshauona, hivyo anaona timu itajifunza kutokana na walichokiona katika mzunguko wa kwanza.
  Kocha Hall aliwaaga wachezaji na benchi la ufundi, mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.  

No comments:

Post a Comment