07 November 2013

SIMBA SC YAMALIZIA HASIRA KWA ASHANTI



 Na Ester Maongezi
Timu ya Simba jana ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibamiza Ashanti United, mabao 4-2 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi 24 ikiwa nafasi ya nne nyuma ya Yanga yenye pointi 25 huku, Amis Tambwe akifikisha mabao 10 baada ya kuifungia timu hiyo bao katika mechi hiyo.Katika msimamo wa ligi hiyo, Azam FC inaongoza ikiwa na pointi 26 sawa na Mbeya City ambayo nayo ina idadi ya pointi kama hiyo isipokuwa inazidiwa kwa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Yanga ikikamata nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 25.
Simba ambayo jana iliingia uwanjani ikiwa na uchu wa mabao ilipata bao la kwanza dakika ya saba kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Ramadhan Singano ‘Messi’ baada ya kuwachambua mabeki wa Ashanti.Ashanti baada ya kufungwa bao hilo ilikuja juu ambapo dakika ya 22, Said Maulid alikosa bao la wazi baada ya kubaki na kipa lakini akashindwa kufunga.
  Maulid aliikosesha tena bao Ashanti, dakika ya 31 baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Fakih Hakika, lakini mshambuliaji huyo mkongwe akashindwa kukwamisha mpira wavuni.Simba baada ya kushambuliwa mfululizo ilizinduka kutoka usingizini ambapo dakika ya 37, Amri Kiemba alikosa bao la wazi baada ya kupata pasi ya Jonas Mkude.
  Dakika ya 44 Singano aliikosesha Simba bao la wazi baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Tambwe, lakini shuti la mshambuliaji huyo likadakwa na kipa wa Ashanti.Ashanti ilisawazisha bao hilo dakika ya 45 kupitia kwa Hussein Sued, baada ya kuitumia nafasi vizuri aliyoipata.
  Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kulishambulia lango la Ashanti ambapo dakika ya 46, Tambwe aliipatia Simba bao la pili baada kuunganisha vyema krosi ya Singano ambaye jana alikuwa nyota wa mchezo.Dakika ya 49, Betram Mombeki aliiandikia bao la tatu Simba akiunganisha krosi ya Singano kutoka wingi ya kulia.
  Maulid aliipatia Ashanti bao la pili dakika ya 52 baada ya kuunganisha mpira wa krosi uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Simba akigaagaa bila mafanikio.Simba ilihitimisha bao la nne dakika ya 60 kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya beki wa kulia, Haruna Shamte aliyepanda mbele kuongeza mashambulizi.
Naye Omari Mngindo anaripoti kutoka Uwanja wa Mabatini Mlandizi kuwa, Timu za Mtibwa na Ruvu Shooting zilitoka sare katika mfululizo wa mechi hizo za ligi kuhitimisha raundi ya kwanza.
Ligi hiyo inatarajia kuchezwa tena leo ambapo Yanga itaumana na JKT Oljoro katika Uwanja wa Taifa, huku Azam FC ikiwa wenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment