06 November 2013

NAIBU MEYA KILIMANJARO AFARIKI DUNIA



Na Heckton Chuwa, Moshi
  Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kiboriloni kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Vincent Rimoy, amefariki dunia jana mchana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Meya wa halmashauri hiyo, Mstahiki Jaffari Michael, alisema Rimoy alifariki wakati akikimbizwa hospitali baada ya kudondoka akiwa shambani kwake eneo la Mandaka, Mjini Moshi.
"Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC," alisema Mstahiki Michael pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Moshi Mjini.
Akizungumza na Majira, mmoja wa wafanyakazi wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema Rimoy aliamka asubuhi na kwenda shambani kwake baada ya kutoka safari ya Dar es Salaam Novemba 4, mwaka huu (juzi).
  Naye mmoja wa rafiki zake na marehemu ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kifo cha Rimoy kinaikumbusha familia yake machungu yaliyowakuta miaka 23 iliyopita.
 "Rimoy aliwahi kupata ajali ya gari Sikukuu ya Pasaka mwaka 1990 akiwa na familia yake... katika ajali hiyo alimpoteza mkewe na watoto wote watano, hakika inasikitisha," alisema.
  Mbali ya kuwa mwanasiasa, marehemu  alikuwa akijishughulisha na biashara akimiliki hoteli maarufu Mjini Moshi inayoitwa New Castle, biashara ya ujenzi pamoja na kumiliki Shule ya St. Patrick.

.



   

No comments:

Post a Comment