15 November 2013

MWILI WA DKT. MVUNGI KUWASILI LEO, SHEIN AMLILIA


Makamu wa Rais,Dkt. Mohamed Gharib Bilal,akimfariji Bi.Anna Shayo ambaye ni mke wa marehemu, Dkt. Sengodo Mvungi,wakati alipofika nyumbani  kwa marehemu Kibamba Msakuzi,Dar es Salaam,jana mchana kwa ajili ya kufariji familia ya marehemu na kutoa mkono wa pole. Mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili nchini leo jioni ukitokea nchini Afrika Kusini.


Na Mwandishi Wetu

  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba kutokana na kifo cha Mjumbe wa tume hiyo, Dkt. Sengondo Mvungi (61).


Katika salamu zake, Dkt. Shein ameeleza kusikitishwa kwake na kifo hicho ambacho ni pigo kubwa kwa maendeleo ya Taifa na Watanzania wote.

"Dkt. Mvungi alikuwa mzalendo mwenye upendo mkubwa kwa nchi yake na mtaalamu wa sheria, alikuwa mwanasiasa shupavu na makini.

"Mimi binafsi, wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tumehuzunishwa na kifo chake, natoa rambirambi zangu kwa tume, Mwenyekiti wake, familia, jamaa na marafiki," alisema.

 Wakati huo huo, Mwili wa marehemu Dkt. Mvungi, utawasili nchini leo kuanzia saa 12:50 jioni.

  Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Assaa Rashid, alisema mwili huo utawasili na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

  Alisema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu Dkt. Mvungi, zimekamilika chini ya uratibu wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo.

  "Baada ya kuwasili, utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa, Marehemu Dkt. Mvungi ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kesho.

  "Anatarajiwa kusafirishwa Novemba 17, mwaka huu kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika Novemba 18 mwaka huu," alisema Rashid.

  Dkt. Mvungi alifariki Novemba 12, mwaka huu, katika Hospitali ya Millpark, jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Ki tengo cha Mifupa Muhimbili (MOI), ambako alilazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilayani Kinondoni.

  Watu hao walimjeruhi vibaya kwa mapanga kichwani usiku wa kuamkia Novemba 3, 2013. Hadi sasa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu 10 ambao wanadaiwa kuhusika na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment