15 November 2013

MKE AFANYA MAUAJI TATA

  • ASHIRIKIANA NA MWANAYE KUMUUA MUMEWE
  • KISA WIVU WA MAPENZI,POLISI WAZUNGUMZA


 Na Esther Macha, Mbeya
  Mama na mtoto, wote wakazi wa Kijiji cha Iseche, Kata ya Mwambani, Tarafa ya Kwimba, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, wanatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua Silvester Chikondo (55).

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athuman, alisema marehemu alishambuliwa kwa marungu na mama huyo ambaye ni mkewe na mtoto wake.
Alisema tukio hilo limetokea Novemba 12 mwaka huu, saa mbili usiku katika Kijiji cha Iseche, wilayani humo.Aliongeza kuwa, marehemu alikutwa na mauti wakati akitoka kilabuni kwenye pombe za kienyeji ndipo mama huyo akiwa na mwanaye wa kiume, walianza kumshambulia.
  Hata hivyo, Kamanda Athumani alisema marehemu alipigwa marungu kichwani na kuongeza  kuwa, mama huyo anaitwa Husulina Kornel (42) na mwanaye Kondo Chikondo (19).
  Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, alisema marehemu alishambuliwa baada ya kufika nje ya nyumba yake ambapo chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa kimapenzi.
  "Marehemu alionekana akizungumza na mwanamke kilabuni ndipo mke wake alipoingiwa na wivu, ugomvi huo ulianzia kilabuni, mke na mwanaye wamekimbia," alisema.
  Alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kubainika ubongo kuchanganyika na damu hivyo kusababisha kifo chake.
Hata hivyo, Kamanda Athumani ametoa wito kwa jamii hasa wanandoa, kutatua matatizo yao kwa njia ya mazungumzo si kujichukulia sheria mkononi kinyume cha sheria.
  Alitoa wito kwa watu wenye taarifa za watuhumiwa, wazitoe ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Pia amewataka watuhumiwa hao, wajisalimishe wenyewe.

No comments:

Post a Comment