28 November 2013

MTOTO MWINGINE WA MANGULA AFARIKI,JK AMLILIA



 Na Mwandishi Wetu
  Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, kufuatia kifo cha mtoto wake, Peter Philip Mangula, kilichotokea juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.

"Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha mwanao (Peter Philip Mangula)," alisema kwa masikitiko Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais Kikwete aliongeza kusema kuwa; nasikitishwa zaidi na taarifa za kifo hiki kwa kuzingatia kwamba ni katika kipindi kifupi kilichopita, Mangula alimpoteza binti yake, Neema Nemela Mangula aliyefariki dunia kutokana na ajali ya gari, hivyo ni dhahiri kwamba kifo cha kijana wake huyu kimeongeza machungu na simanzi kwa familia ya Mangula na kimesababisha pengo kubwa kwa wanafamilia kwa ujumla.
"Kutokana na taarifa hizo za kusikitisha, ninakutumia wewe salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwako wewe binafsi na kwa familia yako yote kwa ujumla kwa kupotelewa na mtoto wako."
Alisema anamuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mjalie yeye na familia yake moyo wa uvumilivu na ujasiri ili kuhimili machungu ya kuondokewa na kijana wao.  

1 comment: