28 November 2013

KILI STARS KUINGIA MZIGONI LEO Na Mwandishi Wetu, Nairobi
  Timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro leo inashuka uwanjani kumenyana na Zambia, katika mechi ya ufunguzi ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Kilimanjaro Stars na Zambia zitachuana kuwania pointi tatu katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Machakos ulioko nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Timu hiyo ya Tanzania Bara iliyopangwa Kundi B, inahitaji ushindi ili kupata pointi tatu ambazo zitaiweka katika nafasi nzuri kwenye michuano hiyo.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Kili Stars, Kim Poulsen alisema timu yake imejiandaa vyema kwa mchezo huo.
Alisema kikosi chake kimefanya ma z o e z i ma g umu , amb a y o yataiwezesha kutoa upinzani dhidi ya Zambia inayosifika kwa kutandaza soka ya kiwango bora Afrika.
“Tumejipanga vizuri nina matumaini vijana wangu hawataniangusha na watafanya vyema kwa kuanza michuano vizuri,” alisema Kim.
Kocha huyo raia wa Denmark alisema mbali na maandalizi hayo, anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa Zambia ni timu imara ambayo, imekuwa ikifanya vyema katika michuano mbalimbali.
Lakini alisema wachezaji wake wanaweza kupata changamoto kwa kuwa uwanja utakaotumika kwa mchezo huo una nyasi za kawaida.
Alisema Kilimanjaro Stars imekuwa ikitumia nyasi za bandia katika maandalizi ya mechi zake kwenye Uwanja wa Karume au Taifa, Dar es Salaam.
Kilimanjaro Stars itawategemea wachezaji kama Mrisho Ngasa, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Said Morad, Athuman Idd na Salum Abubakar.
Pia, wamo Frank Domayo, Himid Mao, Haruna Chanongo, Ramadhan Singano ‘Messi’, Farid Mussa na Elias Maguli.
Katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa jana mchana timu ya taifa ya Zanzibar iliifunga Sudan Kusini mabao 2-1 katika mchezo mkali uliokuwa na ushindani.

No comments:

Post a Comment