26 November 2013

MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMPIGA MAPANGA MTOTO



 Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Bw. Ronginus Haule (58), mkazi wa Madizi Lizaboni, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kumpiga mapanga mtoto Benson Nilah (5) aliyekwenda katika bustani yake kuchuma mapera, anaripoti Cresensia Kapinga, Songea.

Majeruhi huyo ni mtoto wa Mwandishi wa Habari na Mtangazaji wa Kituo cha Radio Maria, wilayani Mbinga, Bw. Geofrey Nilah, ambapo tukio hilo lilitokea Novemba 22 mwaka huu, saa 12:30 jioni, kwenye Mtaa wa Madizini Lizaboni.
Akizungumza na Majira ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi, alisema inadaiwa siku ya tukio mtoto huyo alionekana kwenye gofu la nyumba akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Alisema taarifa za tukio hilo zilifikishwa Kituo Kikuu cha Polisi na Mwenyekiti wa Mtaa wa Madizini, Addo Mkanula ambaye alimfikisha mtoto huyo kituoni na kupewa fomu ya matibabu PF3 ili aweze kuwahishwa hospitali ya mkoa.
“Baada ya kufikishwa hospitali, hali yake ilionekana kuwa mbaya hivyo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa ambao wanahitaji uangalizi maalumu (ICU), kwa matibabu zaidi.
“Hadi sasa, hali yake si nzuri sana, madaktari wanaendelea kumpa matibabu, tukio hili limewashtua wakazi wengi wa Manispaa hii,” alisema Kamanda Malimi.
Aliongeza kuwa, sababu za kumshikilia mtuhumiwa ni baada ya kupata taarifa za kina kuwa mtoto huyo aliingia katika bustani yake kuchuma mapera, ndipo Bw. Haule alimuona na baada ya kumkamata, alianza kumpiga kwa kitu chenye ncha kali.
Hata hivyo, kamanda Malimi alisema kuwa polisi wanaendelea kumhoji Bw. Haule na kutafuta ushahidi zaidi wa tukio hilo na ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

No comments:

Post a Comment