Na Mwandishi Wetu
Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa kampuni huru
za minara ya mawasiliano ya simu, kunaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa
kampuni za simu za mkononi nchini, hivyo kuweza kusaidia kuleta ahueni kwa
watumiaji wa simu hizo.
Kabla ya hapo kampuni zote za simu za mkononi nchini kila
moja ililazimika kujenga mnara wake ambao unahitaji kiasi kikubwa cha uwekezaji
ikiwa ni pamoja na matumizi ya jenereta, ulinzi na gharama nyingine za
uendeshaji.
Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa
Kampuni ya Helios Towers, Michael Magambo wakati akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam.
"Hapo ndipo kampuni huru za minara zinapoingia.
Humiliki, husimamia na huendesha minara, inayoweza kutumiwa na kampuni nyingi
za simu kwa wakati mmoja na pia hata matangazo ya Tv, redio na mawakala wa hali
ya hewa," alisema.
Alisema, matumizi ya mnara
mmoja huondoa mzigo wa gharama za uwekezaji wa miondominu pamoja na shughuli
nyingine kwenye eneo la mnara.
Pia alisema, kampuni za
simu zinapata nafasi ya kuelekeza nguvu zaidi katika eneo wanaloliweza zaidi
kutoa huduma za sauti na 'data' kwa Watanzania.
"Wengi hawaufahamu
mchango wetu katika kupanua huduma za simu Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Helios Towers ni kampuni kubwa ya minara huru nchini, ikiwa imejenga zaidi ya
minara 1,000 ya Tigo Tanzania
mwaka 2010, kisha ikajenga minara mingine 250 na inatarajia kuongeza mingine
150 ifikapo Desemba mwaka huu," alisema Magambo.
Aidha, alisema kwa miaka
miwili iliyopita, maeneo ya Helios yanayotumiwa kwa pamoja na kampuni za simu
ni asilimia 53 kwa sasa na ni asilimia 60 ya maeneo mapya kwa nchi nzima huku
ikisubiri uthibitisho wa serikali wa kuchukua minara ya Vodacom Tanzania.
"Tumekuwa tukisikia wakosoaji wakidai kwamba, kampuni kama Helios hayana ushindani kwa kuwa yamekamata soko
kubwa.
"Hii si kweli.
Uhakika ni kwamba Helios imekuwa chachu ya kuwapo kwa ushindani kwenye soko la
huduma za simu, ikiruhusu wageni kuingia kwenye soko na kuwapa nafasi watoa
huduma kupeleka vijijini bila wasiwasi.
"Mwishowe ni walaji
ndio hufaidika zaidi kwa kupunguziwa bei za simu na kuchagua mtandao
wanaoutaka. Ukweli ni kwamba tunafungua zaidi soko," aliongeza Magambo.
Hata hivyo, katika
kupunguza changamoto za kupeleka huduma maeneo ya vijijini yasiyo na huduma za
simu, awali Serikali ilitoa gari lijulikanalo kama
Universal Communication Action Fund (UCAF) linalosaidia kupunguza gharama na
kuwahamasisha watoa huduma kwenda kwenye soko la vijijini.
Hatua hiyo ilitokana na
Sheria ya Upatikanaji wa Mawasiliano ya mwaka 2006 yenye lengo la kukuza
maendeleo ya kijamii na uchumi mijini na vijijini kupitia TEKNOHAMA.Mbali na
hayo Kampuni ya Helios iko mbioni kuweka mitambo 27 chini ya UCAF
No comments:
Post a Comment