Na Mwajuma Juma, Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar, linamtafuta ofisa mmoja wa Bandari
ambaye anatuhumiwa kuhusika na usafirishaji meno ya tembo kupitia Bandari ya
Malindi, visiwani humo.
Mbali ya kumsaka ofisa huyo, pia jeshi hilo limeanza kuwahoji
baadhi ya watu na kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili kuwabaini
wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema watu wawili wanashikiliwa hadi sasa ambapo
ofisa huyo wa Bandari bila kumtaja jina lake, anaendelea kutafutwa.
Alisema kazi ya kupakua mzigo na kuhesabu meno hayo tayari
imekamilika ambapo kinachoendelea ni kufanya majumuisho ili kujua thamani
halisi ya meno yaliyokamatwa.
"Vipande 1,021 vya meno ya tembo ndiyo vilivyokamatwa
vikiwa katika magunia yenye uzito wa kilo 2,915, meno haya yalikuwa
yasafirishwe kwenda nje ya nchi," alisema Kamishna Mussa.
Hata
hivyo, alisema kuwa watu wawili wanaoshikiliwa wamekuwa wakirushiana mpira kila
mmoja akimuhusisha mwenzake na mzigo lakini hadi jana, wahusika wa mzigo huo walikuwa hawajakamatwa.
"Watu wawili tunaowashikilia, mmoja anahusika na kampuni iliyokuwa
isafirishe mzigo huu ya Island Sea Shells CO. LTD, tunaendelea kufanya
uchunguzi ili kufahamu kama imesajiliwa Zanzibar
au nje na wamiliki wake," alisema.
Aliongeza kuwa, kumetokea utata mkubwa juu ya nyaraka zilizokuwa
zitumike kusafirisha mzigo huo ambao ulikuwa umehifadhiwa katika eneo la
Darajabovu na baadaye kusafirishwa kwa gari hadi ndani ya Bandari ya Zanzibar.
"Kuna
mambo ya kutatanisha yamejitokeza kuhusu nyaraka za usafirishaji wa mzigo huu,
tutaliweka wazi baada ya uchunguzi kukamilika,", alisema Kamishna Mussa.
Alisema wingi wa mzigo huo, haujawahi kutokea Afrika
Mashariki ambapo hilo ni tukio la tatu kutokea Zanzibar. Awali
ilikamatwa kontena la meno ya tembo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na tukio la pili
lilitokea mwaka 2012 katika bandari ya Malindi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment