Na Wilhelm Mulinda, Mwanza
Waziri wa Ujenzi, Dkt.
John Magufuli, jana aliweka jiwe la msingi kwenye daraja la waenda kwa miguu,
katika eneo la Mabatini jijini Mwanza na kutupa kijembe kwa vyama vya upinzani
vinavyodai daraja hilo linajengwa kwa gharama yao.
Akihutubia wananchi waliohudhuria tukio hilo,
Dkt. Magufuli alihoji kuwa, kama daraja hilo
linajengwa kwa gharama yao
mbona hawakuweka jiwe la msingi wala kuhudhuria katika shughuli hiyo, hali
iliyofanya wananchi kumshangilia.
Aliwaomba wananchi kumpuuza mtu yeyote ambaye atadai daraja
hilo ni lake bali
linajengwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutumia pesa za
wazalendo.
Alisema ujenzi wa daraja hilo ni miongoni mwa ahadi za zilizotolewa na
CCM kwenye ilani yake ya uchaguzi 2010 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya
barabara nchini.
"Maendeleo hayana chama, Serikali iliyopo madarakani
inatekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wote bila kujali rangi wala
itikadi za vyama zao, vyama vya siasa vinakuja na kupita lakini nchi iko
palepale," alisema.
Awali akisoma taarifa ya mradi wa daraja hilo,
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo, Mhandisi Leonard
Kadashi, alisema ujenzi wa daraja hilo
unafanywa na Kampuni ya Ujenzi ya Nordic kutoka Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, TANROADS
mkoani humo, walishauri ujenzi huo baada ya watu wengi kupoteza maisha kwa
kugongwa na magari wakati wa kuvuka barabara eneo hilo ambalo lina watu wengi.
Alisema mwaka huu, watu 12 wameshapoteza maisha kwa kugongwa na
magari na wengine kupata ulemavu kutokana na ajali za mara kwa mara.
Katika
hatua nyingine, Dkt. Magufuli alisema Serikali ina mpango wa kutengeneza njia
nne kwenye Barabara ya Mwanza- Uwanja wa ndege jijini humo ili kukabiliana na
msongamano wa magari.
No comments:
Post a Comment