Na Mwandishi Wetu
Mashabiki wa Simba na Yanga kwenye miji ya
Tunduma na Morogoro nao, wanatarajia kupata fursa ya kuburudika katika michezo
mbalimbali kupitia bonanza maalumu la Nani Mtani Jembe, lililoandaliwa na
Kilimanjaro Premium Lager litakalofanyika Uwanja wa Mwaka mjini Tunduma na
Kiwanja cha Ndege mjini Morogoro keshokutwa.
Mratibu wa mabonanza hayo, Lawrence Andrew alisema Dar es Salaam jana kuwa michezo mbalimbali ikiwemo soka la
wachezaji saba kila upande, kuvuta kamba na pia mpira wa mezani maarufu kama fussball itapamba mabonanza hayo.
"Burudani mbalimbali pia zitapamba bonanza
litakalofanyika Tunduma, ikiwemo muziki kutoka bendi ya High Class pamoja na
wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wa mkoani Mbeya.
Alisema kwa Mkoa wa Morogoro bendi ya mkoani humo ya Beacon
Sound, itatoa burudani kwa mashabiki watakaojumuika kushiriki bonanza hilo, huku wasanii wa
kundi la dansi GYT wakilishambulia jukwaa.
Mratibu huyo alisema pia
kutakuwa na michezo mbalimbali ya kujifurahisha kama
kufukuza kuku wa kienyeji, kukimbia na gunia na mtu kupiga penalti akiwa
amefungwa kitambaa usoni.
Alisema mabonanza hayo
yanayotarajiwa kuanza saa 3 asubuhi ni mwendelezo wa kampeni ya Nani Mtani
Jembe ambayo ilizinduliwa Oktoba 2, mwaka huu na inafanyika nchi nzima
ikiwashirikisha mashabiki wa timu za Simba na Yanga.
Andrew alisema kupitia
kampeni hiyo, Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini Simba na Yanga imetenga
sh. milioni 100 na kisha kuzigawa kwa timu hizo, ambapo kila moja inazo sh.
milioni 50 ambazo zinashindaniwa na mashabiki wao.
Naye Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro, George Kavishe alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanatakiwa
kushindana kwa kushiriki kwenye kampeni hiyo, ili kuhakikisha kuwa timu
mojawapo inapata fedha nyingi zaidi ya timu nyingine.
Kwa
mujibu wa Kavishe matokeo ya uwiano wa fedha zinavyopungua kutoka Simba au
Yanga, yatatangazwa kila siku hadi siku ya mwisho wa mashindano hayo Desemba
14, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment