14 November 2013

KIFO CHA MVUNGI CHAMTIKISA JK


Rais Dkt.Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifariji familia ya Marehemu Dkt. Sengodo Mvungi nyumbani kwao Kibamba Dar es Salaam jana.
  • SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZAZIDI KUMIMINIKA
  • MWILI WAKE KUWASILI KESHO,KUAGWA JUMAMOSI

 Na Waandishi Wetu
  Rais Jakaya Kikwete, amesema ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, kilichotokea juzi kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini.

Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, Rais Kikwete alisema amepokea kwa mshtuko mkubwa na taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi.
"Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni kubwa," alisema Dkt. Kikwete. Rais Kikwete alisema hakuna shaka kuwa katika maisha yake Dkt. Mvungi alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa kusaka Katiba mpya.
"Kuanzia alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers, hadi uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wa kugombea Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt. Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Na hili sitalisahau," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Kwa masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu nikiomboleza kifo cha Dkt. Mvungi.
“Nakupa pole nyingi wewe Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa Tume kwa kuondokewa na mwenzenu. Naungana nanyi kuombleza msiba huo mkubwa.
“Kupitia kwako, natuma pole nyingi kwa wana-familia, ndugu, marafiki na majirani wa Dkt. Mvungi kwa kuondokewa na mhimili, msimamizi wa familia na ndugu.
“Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu awape subira waweze kuvuka kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Mbatia anena
Wakati huo huo, mwili wa Dkt. Mvungi unatarajia kuwasili nchini kesho na utapokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kisha kupelekwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema baada ya mwili huo kuwasili itafanyika misa takatifu katika Kanisa la Mt. Joseph saa nne asubuhi Jumamosi.
Alisema baada ya misa hiyo saa sita mchana mwili wake utapelekwa viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuagwa na kisha kusafirisha kwenda Mwanga, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.
Alisema katika kipindi hiki cha msiba bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa wiki moja.
Waziri Chikawe
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema msiba huo ni pigo kwa taifa kwani marehemu alikuwa ni kiungo muhimu na alitumia ujuzi, elimu na nafasi aliyonayo kwa jamii hasa katika kipindi hiki muhimu cha mchakato wa katiba mpya.
Alisema ni wananchi waelewe kuwa ikitokea kuyumba au kuwepo kwa pengo lolote katika mchakato huo basi litakuwa limechangiwa na kutokuwepo kwake Dkt. Mvungi.
Jaji Warioba amlilia
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba, alisema Dkt. Mvungi ni mtu muhimu ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwenye Tume yake.
Alisema alitumia utaalam wake wa sheria na uzoefu katika kuhakikisha hoja zake alizokuwa akizitoa anazisimamia ipasavyo.
CUF yatuma rambirambi
Kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kimepokea kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa ya kifo
 cha Dkt. Mvungi.
"Kifo cha Dkt.Mvungi kimeishtua Tanzania nzima hasa kwa vile tulitazamia kuwa angeishi kwa muda mrefu zaidi.
Kifo hicho kinazidi kusikitisha kwa vile kimetokana na kushambuliwa kikatili na watu wasiojulikana wanaodaiwa kuwa ni majambazi," ilieleza taarifa ya CUF.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi CUF, mimi mwenyewe na viongozi waandamizi wa CUF walimjua vizuri sana Marehemu Dkt. Mvungi kwani tulifanya kazi naye kwa karibu," alieleza taarifa ya CUF iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Maalim Seif, alisema Dkt. Mvungi alikuwa mpambanaji jasiri asiyeyumba katika mapambano ya kuiletea Tanzania mfumo wa kidemokrasia halisi unaolenga kulinda haki za kila Mtanzania bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile.
Alisema Dkt. Mvungi alichukia uonevu, manyanyaso, ukandamizaji na dhuluma dhidi ya binadamu yoyote.
"Tulishirikiana naye kwa karibu katika mchakato wa kudai Katiba mpya ya Tanzania na pale vyama vya siasa vilipounda kamati ya kufanya rasimu ya Katiba mpya Marehemu Dkt. Mvungi ndiye aliyekuwa Mwanasheria wa Kamati hiyo.
Alitoa mchango mkubwa katika kuandaa na kukamilisha rasimu hiyo," alisema Maalim Seif na kuongeza;
"Wengi tulifarijika pale alipoteuliwa kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Tulijua uwezo wake, umahiri wake, utendaji kazi makini wake na dhamira yake ya kuona Tanzania inapata Katiba nzuri kwa masilahi ya wananchi wote bila kujali itikadi za vyama."
Alisema Dkt. Mvungi alikuwa ni wakili mahiri, msomi makini na kiongozi shupavu.
Alisema alikuwa jasiri hasa katika kuwatetea wanyonge na katika kutoa mawazo yake. Alikuwa ni mchambuzi hodari wa mambo ya kisheria, hasa sheria inayoambatana na masuala ya Katiba.
Hali kadhalika alikuwa mchambuzi aliyebobea katika masuala ya kijamii na ya kisiasa na aliguswa sana na umuhimu wa kuendeleza elimu bora nchini Tanzania.
Maalim Seif alisema kifo chake ni pigo zito kwa familia yake, Chama cha NCCR-Mageuzi, Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa jamii nzima ya Watanzania.
"Kwa niaba ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF na Wanachama wote wa CUF na kwa niaba yangu mwenyewe, tunatoa mkono wa tanzia kwa familia ya Marehemu, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wafiwa wote," alisema.
CCM yatoa pole
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesikitishwa na kifo cha Dkt. Mvungi na umeonya kuwa umaskini usifanye Watanzania kuwa chanzo cha kuua watu wengine.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkuu wa Idara ya Hamasa na Chipukizi wa UVCCM Taifa, Paul Makonda, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba huo.
"Umaskini wetu wa kipato, akili na mawazo, usiwe sababu ya kuumizana na kugharimu maisha ya mtu kwani hata wale waliomvamia na kumjeruhi huenda wamesukumwa na tamaa zao za kimaisha," alisema.
Polisi yanasa mwingine
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja anayetuhuniwa kuhusika katika tukio la mauaji ya marehemu Dkt.Sengondo Mvungi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa Polisi Kanda, Maalum Suleiman Kova alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi katika maeneo ya Twiga Jangwani.
Kamishina Kova alisema kuwa; "mtuhumiwa alitambuliwa na kukamatwa kisha kuhojiwa na Polisi na alikubali kuhusika katika tukio hilo na askari waliongozana naye hadi nyumbani kwake Kiwalani Migombani ambapo alikutwa na silaha ambayo ni bastola aina ya REVOLVER No.BDN 6111 pamoja na risasi 21 za bastola hiyo ikiwa ni mali ya Dkt.Mvungi,"alisema Kova.
Pia katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi katika chumba cha mtuhumiwa vilipatikana baadhi ya vifaa vya mlipuko vya aina tofauti vikiwemo,baruti aina ya Explgel, Tambi mbili ambazo ni viwashio vya baruti pamoja na mlipuko.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa alipohojiwa kuhusu umiliki wa silaha hiyo alikiri kuwa hana kibali cha kumiliki silaha. Alisema silaha hiyo ni miongoni mwa vitu vilivyoibwa kwa Dkt. Mvungi.

No comments:

Post a Comment