15 November 2013

KIM AITA 16 KUTOKA FUTURE TAIFA STARS



Na Fatuma Rashid
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameunda kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya (Harambee Stars) itakayochezwa Jumanne, Novemba 19, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa wiki ijayo dhidi ya Kenya 'Harambee Stars' katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya mechi hiyo ya kirafiki, wachezaji wa Zanzibar watakwenda kuungana kikosi cha Zanzibar Heroes, wakati wachezaji wa Tanzania Bara watakwenda kupiga kambi Arusha kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Chalenji inayotarajia kuanza Novemba 27 mwaka huu nchini Kenya.
  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kikosi hicho kinajumuisha wachezaji 16 walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.
  Alisema wachezaji wengine 16 wanatoka Future Taifa Stars. Awali kambi ya Future Taifa Stars iliyoanza Novemba 9 mwaka huu na kuvunjwa jana asubuhi ilikuwa na wachezaji 30.
  Wambura aliwataja walioitwa ni makipa wanne; Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Deogratias Munishi (Yanga) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting), Nadir Haroub (Yanga) na Said Moradi (Azam).
  Alisema wengine walioitwa ni viungo wakabaji Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) na Vincent Barnabas anayechezea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
  Wambura aliwataja wengine kuwa ni viungo Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na William Lucian (Simba).
  Wengine ni viungo washambuliaji ambao ni Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Mrisho Ngassa (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Markhiya, Qatar) na Simon Msuva (Yanga).
Aliwataja washambuliaji kuwa ni Elias Maguli (Ruvu Shooting), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) Mbwana Samatta (TP Mazembe, DRC) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

No comments:

Post a Comment