Na Mariam Mziwanda
Muungano wa Tanzania na Zanzibar umefananishwa na mgonjwa aliyelazwa
kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), hivyo Watanzania wametakiwa
kuunusuru kupitia Katiba Mpya inayotarajiwa kupatikana kabla ya uchaguzi mkuu
ujao mwaka 2015.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utetezi na
Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia,
wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa asasi za kiraia.
Alisema ni muhimu kwa wananchi kupewa fursa ya kujadili
Muungano na kuufahamu kwa kina kuwa unahitajika ili kuepukana na chuki
zinazopandikizwa kutoka kwa wanasiasa wenye uchu wa madaraka.
“Kuna wanasiasa wachache wanaotumia nafasi zao ndani ya
jamii kupotosha wananchi kuhusu muungano, wanapandikiza chuki kwa ahadi za
kisiasa ili wapate madaraka,” alisema.
Aliongeza kuwa elimu ya faida za Muungano ikiwafikia vizuri
wananchi na kupewa fursa ya kujadili ipasavyo kwa muda uliopo kabla ya Bunge la
katiba inatosha kuufanya hudumu na kuwa matunda kwa vizazi vijavyo.
Alisema Muungano uliopo unategemea kufa au kupona kutokana na
maamuzi ya nchi kupitia katiba mpya kwani umegubikwa na kero nyingi ambazo kwa
muda mrefu hazijapatiwa tiba.
“Muundo wa Muungano ni tatizo hususani katika uundaji wa Serikali
yenyewe hali inayosababisha wananchi wa pande zote mbili kulalamika, lakini
wakati uliopo unatosha kupitia Bunge la katiba kunusuru muungano ulipo,”
alisema.
Akileleza changamoto kubwa ambazo wananchi wanatakiwa kuzipatia
majibu kupitia katiba mpya ili kuwa nyenzo ya uhai wa Muungano huo alisema ni
pamoja na utatuzi wa suala la mapato katika mgawo wa asilimia nne kwa Zanzibar
na uwepo wa uhuru wa kuchagua viongozi.
Kwa upande wa mjumbe wa AZAKI takriban 36, Baraka Mohamed Shamte,
alisema Watanzania bado wanahitaji Muungano na kwamba jambo la muhimu ni
kujadili matatizo yaliyopo na kuyafanyia kazi ili uendelee kudumu.
“Kuanzishwa kwa Muungano hakukuwa kwa bahati mbaya historia ya
Muungano wananchi wake ni wamoja, vijana wa leo wakishasoma na kupata shahada
wanafikiri wanafahamu kila kitu, kulikuwa na sababu tosha za kuungana kwa nini
Muungano huo haukuwa na Kenya nchi nyingine ni vyema kuwa wa kweli katika
kuzungumzia Muungano,” alisema.
Kwa upande wake Ramadhan Suleiman Nzori
aliwataka vijana wasomi kutambua kuwa wanategemewa sana katika kulinda na kuthamini Muungano na
wasichukue vitu vidogo vidogo na kuona ni rahisi kuvunja Muungano uliopo.
No comments:
Post a Comment