12 November 2013

MANUMBA ASTAAFU RASMI AJIRA POLISI   Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, amestaafu rasmi kazi kwa mujibu wa sheria baada ya kufikisha umriwamiaka 60.Katika utumishi wake ndani ya Jeshi la Polisi, amefanya kazi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo chumba cha kupokea mashtaka kuanzia mwaka (1976-1977).

  Nafasi nyingine ni Mwendesha Mashtaka Wilaya ya Kibondo na Kasulu, mkoani Kigoma (1977- 1984), Mkufunzi wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam, (1984-1987), Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Magomeni, Kinondoni na Naibu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (1987-1993),
  Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Msemaji wa jeshi hilo, SSP Advera Senso, ilisema Manumba pia aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi mkoani Arusha (1993- 1995), Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi (1995-1996) na Mkuu wa Kitengo cha Fraud Makao Makuu ya Upelelezi (1996-1997).
  Nafasi nyingine Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Nchi, Intelijensia na Dawa ya Kulevya Makao Makuu ya Upelelezi (1997- 2001) na Msaidizi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (2001-2006).
 Alisema kuanzia 2006 hadi anastaafu, alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI).Mkuu wa jeshi hilo nchini, IGP Said Mwema, amemshukuru Manumba kwa kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbalimbali ndani ya jeshi hilo kwa weledi na uaminifu mkubwa wakati wote wa utumishi wake.
  Alimtaka aendelee kuwa msaada kwa jeshi hilo, kutoa ushirikiano wa namna yoyote unaoweza kupunguza uhalifu nchini kwa sababu suala la usalama ni taaluma kama zilivyo taaluma zingine na taaluma hiyo wanayo watu wachache.
  SSP Senso alisema, wakati taratibu za uteuzi wa DCI mpya zikiendelea, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini CID Makao Makuu, Kamishna Isaya Mungulu, atakua akikaimu nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment