Na Fatuma Rashid
Klabu ya Yanga imeiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi pamoja na Manispaa ya Ilala, kujibu barua yao
kuhusu kuomba eneo la nyongeza ili kukamilisha azma yao
kujenga uwanja ambao utajulikana kwa jina la Jangwani City
utakaokuwa na miundombinu yote
. Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya uwanja huo, Francis Kifukwe
alisema barua ya kuomba eneo la nyongeza iliandikwa Desemba 12 mwaka jana,
lakini mpaka sasa bado hawajapata jibu.
Kifukwe alisema mpango wao katika ujenzi wa
uwanja wa kisasa wa Yanga ni kuboresha mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza
mazingira na miundombinu.
"Tunahitaji eneo hili liwe na sura ya
kibiashara na kitalii, ambapo tutahitaji kudhibiti mafuriko ambapo pia tutajaza
udongo (kuweka tuta kubwa), upandaji miti, bustani za kubarizi na kuboresha
mifereji ya maji taka," alisema.
Alisema kutokana na kukua kwa jiji na katika
hali ya kutaka klabu iwe na vitegauchumi, wameonelea ni vizuri kama ingekuwa na
uwanja wa mpira wa kisasa utakaochukua watazamaji elfu 40.
Aliongeza kuwa pia kutakuwa hosteli kwa ajili
ya wachezaji, uwanja wa mazoezi, eneo la kuegesha magari, hoteli na sehemu ya
makazi, ukumbi wa mikutano, ofisi, benki, zahanati ya wachezaji, supermarket na
sehemu za kujipumzisha.
Aliongeza kuwa mara baada ya azma hii
kukamilika eneo hili litafahamika kama 'Jangwani City'
na kufanya wakazi wa Jangwani na maeneo ya jirani wasiende maeneo ya mbali
kutafuta huduma muhimu.
Kifukwe alisema makubaliano ya awali
yalisainiwa Novemba 23, mwaka jana ambapo inatakiwa kuwa na eneo la kutosheleza
malengo ya mradi, kupata ushauri, michoro pamoja na mkandarasi mzuri wa miradi
pamoja na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa miradi.
Hivi sasa klabu hiyo ina kiwanja chenye
ukubwa wa hekta 3.59 katika eneo lao la Jangwani ambapo kiwanja hicho kina
hatimiliki kwa miaka 99 kuanzia mwaka 1972.
Katika eneo hilo,
klabu ilifanikiwa kujenga Uwanja wa Kaunda na jengo la klabu lenye ghorofa
tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, pamoja
na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment