01 October 2013

BALOZI SEIF: Z’BAR ILISHIRIKI KATIBA MPYA Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi, amesema kauli aliyoitoa bungeni Mjini Dodoma hivi karibuni juu ya Zanzibar kushirikishwa katika mchakato wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ilikuwa sahihi, anaripoti Mwajuma Juma, Zanzibar.

Balozi Seif aliyasema hayo juzi kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu CCM, mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba akiwa katika ziara yake ya siku mbili kisiwani humo.
Alisema amelazimika kueleza ukweli huo kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake na kambi ya upinzani kudai amekurupuka kutoa kauli hiyo bungeni na kudai kuwa, hapungukiwi kwa lolote.
“Acha waendelee kunitukana na kunikashifu mimi sitopungua, nilichokisema bungeni Dodoma ni sahihi, kuna ushahidi pamoja na kumbukumu zote zinazothibitisha ushiriki wa Zanzibar katika suala hili muhimu,” alifafanua Balozi Iddi.
Balozi Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, mamlaka ya kutunga mswada wa sheria ni kazi ya Serikali ambayo hushirikisha wataalamu na wadau wa sekta zote kazi ambayo inaishia unapowasilishwa katika Kamati ya Bunge.
Alisema Sheria ya Bunge la Katiba ilifikishwa Zanzibar, kujadiliwa na kufanyiwa uchambuzi kupitia wadau wa sekta hiyo waliotoa nyongeza ya baadhi ya vipengele ambavyo vyote vilikubaliwa na kamati iliyosimamia mswada huo.
“Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba imehusisha mambo manne makubwa ambayo ni kuundwa kwa Kamati ya kukusanya maoni, kutungwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Bunge la Katiba na kura ya maoni, mambo haya yalikubalika, kuridhiwa na pande zote za Muungano, ugomvi uko wapi,” alihoji Balozi Iddi.
Akizungumzia uimarishaji wa CCM, aliwakumbusha viongozi na wanachama wa chama hicho Kisiwa Pemba, kuhakikisha wanajenga chama kipindi hiki ambacho ni karibu na Uchaguzi Mkuu 2015.
Aliwataka viongozi wa chama hicho mikoa, kuhakikisha vijana wanaandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura kwani bila kufanya hivyo, hawawezi kupata fursa ya kupiga kura jambo linaloweza kuisababishia CCM mazingira magumu ya ushindi.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mama Asha Suleiman Iddi aliwahadharisha viongozi na wanachama kuepuka tabia ya kuendeleza makundi ndani ya chama hicho.
Alisema tabia hiyo ikiachiwa, inaweza kudhoofisha nguvu za chama na hatimaye kuleta athari katika harakati zake za kujipanga na ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 2015

No comments:

Post a Comment