01 October 2013

WALIPWA MISHAHARA BILA KUFANYA KAZI



Na Yusuph Mussa, Lushoto
  Walimu watano kwenye Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga wanalipwa mishahara wakiwa wametoroka eneo la kazi, huku wengine wakienda kusoma bila kumuaga muajiri wao
  Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani juzi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Patricia Mbigili aliwataja walimu hao watoro kuwa ni William Kilapilo, Wilbert Mbwambo, Juma Vumba, Ali Mwehuti, Abeli Mkope na Ramadhan Mwande.
 "Kilapilo ametoroka tangu 2011, Mbwambo 2012 na Vumba 2012, hawa wote wanafundisha Shule ya Msingi Kwemkomole. Wengine ni Mwehuti 2012 na Mkope 2012 Shule ya Msingi Kwamhe na Mwande wa Shule ya Msingi Kwediwa ametoroka mwaka 2011.
 "Walimu hawa wametoroka eneo la kazi na kwenda kusoma bila utaratibu, lakini tutazingatia maazimio yenu madiwani kuwa tusimamishe mishahara ya walimu hao mara moja," alisema Mbigili ambaye pia ni Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Bumbuli.
  Diwani wa Kata ya Milingano, Ramadhan Hozza ambaye ni mmoja wa walioathirika kwa kutorokwa na walimu alisema elimu ya Tanzania inashuka kwa mambo mengi kwa vile baadhi ya walimu wanatumia ngazi ya kuajiriwa kama sehemu ya wao kwenda kusoma, lakini si kufundisha watoto wao.
 Diwani wa Kata ya Vuga alisema, baadhi ya walimu hawakai kwenye vijiji vyenye shule wanazofundisha, bali mjini, matokeo yake inabidi wapangiwe ratiba ya kuanza kufundisha saa nne kwa vile wanafika wakiwa wamechelewa..

1 comment: