- KUANZIA JULAI MWAKA HUU,TRA YATOA SIKU 14
- WATEJA WENGI KUKOSA MAWASILIANO HASA VIJIJINI
Na
Mwandishi Wetu
Kilio cha Watanzania wengi kutaka tozo ya sh. 1,000 kila mwezi kwa
laini moja ya simu ifutwe, bado kipo mashakani baada ya Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA), kuzitaka kampuni za simu nchini kulipa tozo hiyo kuanzia Julai
mwaka huu ndani ya siku 14.
Awali tozo hiyo ilitakiwa kuanza kulipwa Julai
mwaka huu, lakini kutokana na malalamiko ya wadau, utekelezwaji huo ulisubiri
mapendekezo ya Tume Maalumu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kushughulikia
tatizo hilo.
Hivi karibuni,
Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Simu nchini (MOAT) ulisema asilimia 48 ya
Watanzania ndio wanaotumia simu za mkononi sawa na watu milioni 22.Kutokana na
tozo hiyo, zaidi ya asilimia 40 hadi 45 watafungiwa simu zao na kudai takribani
Watanzania milioni nane, hushindwa kuweka sh. 1,000 kwa mwezi katika laini za
simu zao.
MOAT waliongeza kuwa,
kuendelea kukua kwa sekta ya mawasiliano hasa maeneo ya vijijini, kutakuwa na
mashaka kwani wengi wao watashindwa kumudu gharama za simu hivyo kukwamisha
malengo ya Umoja wa Kimataifa katika maendeleo ya mawasiliano. Tume iliyoundwa
na Rais Kikwete ilijumuisha wajumbe kutoka TRA, Wizara ya fedha na wawakilishi
wa kampuni za simu
Julai 19 mwaka
huu, Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, alisema Serikali imekubali kupitia
mawazo na maoni ya MOAT kuhusu kufutwa kwa tozo hiyo ambayo imelalamikiwa na
wadau wengi wa sekta ya mawasiliano.
Hali hiyo
ilitokana na kauli za baadhi ya viongozi wa Serikali, wabunge na wananchi
wanaopinga tozo hiyo wakidai huo ni mzigo kwa watumiaji simu hasa wa kipato cha
chini.
Dkt. Mgimwa alisema
walikutana na MOAT na kupokea mapendekezo yao
ambayo wanayafanyia kazi ili tupunguze makali ya kodi hiyo kwa wananchi wa hali
ya chini. Alionya kusiwepo na jazba kwani suala hilo ni la kisheria kwa sababu lilipitishwa
bungeni hivyo ili kuondolewa lazima ufuatwe
utaratibu kwani hakuna mtu anayelenga kumkamua mwananchi.
Alisema kodi hiyo ilitokana na mapendekezo 67
yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti kuwa chanzo cha mapato kinachotekelezeka
lakini kama inaonekana kikwazo, wataliangalia
jinsi ya kukabiliana nalo
Aliongeza kuwa lengo la tozo hiyo ni
kupata fedha ambazo zitaelekezwa katika miradi ya maji, barabara na umeme hasa
vijijini ambako kuna changamoto nyingi za maendeleo.
Alisisitiza kuwa, hakuna
mtumiaji wa simu ambaye ameanza kukatwa tozo hiyo kutokana na mchakato huo kuwa
bado unaendelea katika utekelezaji wake
Naye Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema Serikali itahakikisha mwananchi
hapati mzigo usiokuwa na sababu.
Aliongeza kuwa, Serikali ni sikivu na inawasikiliza wananchi wake,
hivyo kupitia mawazo na mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa, yatafanyiwa kazi
ili kutokuathiri pande zote.
No comments:
Post a Comment