17 October 2013

VYAMA VYA SIASA VYAMSHUKIA ZITTO


  •  KILA CHAMA CHAMVAA KWA STAILI YA AINA YAKE
  • VYAMTAKA AACHE KULAZIMISHA KUTAFUTA UMAARUFU
Na Darlin Said

  Vyama vya siasa vya CCM, CUF na NCCR-Mageuzi vimemshukia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, kutokana na kauli yake ya kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, kusitisha ruzuku kwa vyama hivyo kutokana na kushindwa kuwasilisha hesabu za fedha tangu mwaka 2009.


Vyama hivyo vimemtaka Zitto aache kukurupuka na kulazimisha kutafuta umaarufu kwa kuandikwa kwenye vyombo vya habari.Kauli ya vyama hivyo, imekuja baada ya kamati ya PAC kudai kuwa kukutana na Jaji Mutungi na kushindwa kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP na vyama vingine vya siasa. Kutokana na hali hiyo, Zitto alishauri ruzuku ya vyama hivyo isitishwe.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alimtaka Zitto, atoe kwanza boliti kwenye macho yake ndipo aweze kuona kibanzi kilichopo kwenye macho ya mwenzake.

Alisema CHADEMA n i miongoni mwa wahusika ambao hesabu zao hazijakaguliwa, kwani ndicho kimekuwa kikilalamikiwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.Alisema chama chake hakihusiki kwani kimekuwa kikitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Alisema kwa mwaka 2009 hadi 2011 mahesabu ya CCM yalikuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje (TAC) na kwamba Januari, mwaka huu, CCM iliiandikia barua ofisi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya kuwasilisha rasimu ya hesabu za fedha za mwaka 2011/2012 kwa lengo la kumtaka apangie chama hicho mkaguzi.

Alisema CAG alipangia TAC akague hesabu za chama hicho ambaye alifanya kazi hiyo, hivyo chama hicho akihusiki."Hesabu zote zilizokaguliwa zimewasilishwa kwa CAG, hivyo CCM haihusiki na agizo hilo na muda wowote PAC akizihitaji itazipata," alisema Nape.

Alishauri vyama ambavyo PAC itabaini havikuwasilisha mahesabu yake viongozi wake wawajibike.Kwa upande wa CUF, chama hicho kimesema Zitto amekurupuka kwa kuwa hana taarifa za kutosha na hajui kinachojiri. "Mwenye jukumu la kufuatilia hesabu hizo ni CAG ambaye hatujawahi kumsikia akilalamika," alisema Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro.

Alisema CUF kila mwaka imekuwa ikifunga mahesabu kwa kukaguliwa na wakaguzi wa ndani na nje, lakini hawajawahi kuona watu wa Serikali wakienda kukagua hesabu hizo.Mtatiro alisema kuwa mwaka 2011 Serikali iliiandikia barua CUF ya kupelekewa mkaguzi ambaye chama hicho kilitakiwa kumlipa, lakini walikataa.

"Tulijibu kuwa hilo haliwezekani kwa kuwa hilo ni jukumu la Serikali, kuanzia hapo hatukuwaona tena... hivyo Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake," alisema.Mmoja wa viongozi wa NCCR-Mageuzi, aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, alisema kauli ya Zitto ni ya kutafuta umaarufu kupitia vyombo vya habari na inaonekana haelewi kinachoendelea.

Awali vyama vilikuwa vikifanya mahesabu vyenyewe na kupeleka taarifa serikalini, lakini baada ya sheria kubadilishwa jukumu hilo (ukaguzi) alipewa CAG. Alisema CAG ndiye anabidi aende kufanya ukaguzi huo, lakini tangu sheria hiyo ibadilishwe hawajawahi kumuona.

  Alisema baadaye Msajili wa vyama wakati huo (John Tendwa) aliandikia vyama vya siasa barua ili viwe vinamlipa CAG kwa kazi hiyo ya ukaguzi, lakini vilikataa kwani kufanya hivyo ni sawa na kumlipa mshahara mara mbili, wakati analipwa na Serikali kwa kazi hiyo.

 "Tulihoji iweje anapoenda kufanya ukaguzi kwenye halmashauri alipwe na Serikali, lakini kwenye vyama alipwe na vyama wakati Serikali inamlipa," alisema na kuongeza; "Tangu wakati huo hatujawahi kumuona."

  Alisema sio kweli kwamba vyama vinashindwa kuwasilisha mahesabu, bali CAG ndiye hajafanya hivyo.Alitoa mfano kuwa mahesabu ya NCCR-Mageuzi yapo tayari na kwa kawaida huwa yanakaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho. "Kwa hiyo kamati ya Zitto imekurupuka anatafuta umaarufu kupitia kwenye vyama," alisema.

No comments:

Post a Comment