21 October 2013

SIMBA, YANGA' NGOMA NZITO'Na Elizabeth Mayemba

 Wakongwe wa soka nchini, Simba na Yanga jana zimetoka sare ya mabao 3-3 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ilionekana kujiamini zaidi kipindi cha kwanza na kuwabana wapinzani wao, hasa katika sehemu ya kiungo na kuwafanya wachezaji wa Simba kuutafuta mpira kwa muda mrefu.

Mpira ulianza kwa Yanga kuliandama lango la Simba na kufanya mashambulizi mfululizo lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kutumbukiza mpira kimiani.Simba walizinduka dakika ya 14 ambapo, Said Nassoro 'Cholo' alikosa bao baada ya kuwapangua mabeki wa Yanga na kupiga shuti, lililotoka nje.
  Yanga ilipata bao dakika ya 16 baada ya beki wa Simba, George Owino kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa.Dakika ya 24, David Luhende aliikosesha Yanga bao baada ya kuunasa mpira miguuni mwa Abdulhamud Humudi, ambapo alipiga shuti lililotoka nje ya lango, huku Hamis Kiiza, naye akipiga shuti lililodakwa na kipa Abel Dhaira.
  Kiiza aliipatia Yanga bao la pili, baada ya kuunganisha mpira uliorushwa na beki Mbuyu Twite.Ramadhan Singano 'Messi', aliikosesha Simba bao dakika ya 44 baada ya kupata nafasi nzuri lakini shuti lake likadakwa na kipa Ally Mustafa 'Barthez'.
  Yanga ilipata bao dakika ya 45 kupitia kwa Hamis Kiiza, baada ya kuunganisha pasi ya Didier Kavumbagu.Kipindi cha pili Yanga iliingia na kufanya mashambulizi ambapo dakika 62, Haruna Niyozima aliikosesha Yanga bao la wazi baada ya kupokea pasi nzuri ya Kavumbagu lakini mabeki wa Simba wakaokoa.
  Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 64 kupitia kwa Patrick Mombeki, huku beki George Owino akifunga la pili kwa kichwa akiunganisha kona ya Singano.Amis Tambwe aliisawazishia Simba bao la tatu dakika ya 77 baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na beki, Said Masoud 'Cholo'.
  Dakika ya 40, Simba ilimtoa Mombeki baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Zahoro Pazi. 
  Naye Fatuma Rashid, anaripoti kuwa, baadhi ya mashabiki wa timu hizo walipoteza fahamu, kila bao lilipokuwa likifungwa.Kipindi cha kwanza mashabiki wa Yanga zaidi ya sita walipoteza fahamu baada ya timu hiyo kupata mabao 3.Lakini hali ilibadilika kipindi cha pili ambapo mashabiki wa Simba zaidi ya saba, nao walianza kupoteza fahamu kila ilipokuwa ikipata bao.

No comments:

Post a Comment