17 October 2013

BAKWATA YAKUNWA KIKWETE KUKUTANA NA WAPINZANI IKULU

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu muda mfupi baada ya  kushiriki swala ya Idi iliyofanyika katika msikiti wa Maamur Upanga jijini Dar es Salaam jana asubuhi.


 Na Rachel Balama
  Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limempongeza Rais Jakaya Kikwete, kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni na kujadili maendeleo ya mchakato wa Katiba Mpya kwa amani na utulivu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Shekhe Suleiman Lolila, wakati akitoa salamu za baraza la Idi katika Msikiti wa Aly Farouk jijini Dar es Salaam.
Alisema kitendo cha Rais Kikwete, kukubali kukutana na viongozi hao, kinaonesha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea nchini utafanyika na kumalizika kwa amani na utulivu.
Alisema rais alitumia busara na kuonesha ustaarabu wa hali ya juu, pale aliporuhusu kuanzishwa kwa mchakato mzima wa Katiba Mpya, ambayo itakuwa ndiyo dira na mwongozo wa nchi kwa vipindi vingine vijavyo.
Aidha, aliwataka wale wote wanaosimamia amani wasimame kidete kutekeleza hilo na kuwaonya wale wanaofanya dhuluma, uonevu ili kila Mtanzania popote alipo aweze kufaidi matunda ya amani.
  Oktoba 15, mwaka huu, Rais Kikwete, alikutana na viongozi hao Ikulu, Jijini Dar es Salaam ili kujadili mapendekezo ya kuboresha sheria ya kurekebisha sheria ya mabadiliko ya katiba.
  Shekhe Lolila, aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kusitisha utekelezaji wa mchakato wa kutotahiniwa kwa masomo ya dini katika mitaala ya elimu ya sekondari na pia kufanya mazungumzo na viongozi wa shule zinazoendeshwa na taasisi za dini ili kufikia mwafaka.
  Naye, mgeni rasmi katika Swala ya Baraza la Idi, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, aliwataka Watanzania kwa ujumla kuepuka ushabiki kwa jambo lolote lile ili kudumisha amani.
  Alisema pia ni vyema Waislamu wakadumishe maadili ya dini yao kama wanavyoelekezwa katika vitabu vitakatifu ili kudumisha amani na kwamba Serikali ipo makini kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kuimarika.
  Pia aliwataka Waislamu kutafuta elimu popote pale duniani kwa kuwa Serikali imeweka sera nzuri katika elimu na kuwataka kuongeza michango yao kwa ajili ya elimu ya juu. Alisema kwa sasa michango wanayotoa hailingani na wingi wao.
  Aliwataka viongozi wa dini hiyo wafikirie kuanzisha chuo kikuu kingine katika kanda mbalimbali hapa nchini ili kuandaa vijana na kuzalisha wataalamu.
 "Chuo Kikuu cha Kiislamu kipo kimoja tu Morogoro, hivyo kutokana na wingi wenu hamkustahili kuwa na chuo kimoja tu, jambo ambalo halistahili," alisema Profesa Maghembe.
  Naye, Kaimu Mufti, Shekhe Abibu Makusanya, aliitaka Serikali ioneshe makali kwa kuhakikisha wale wote wanaoonesha ishara mbaya za uvunjifu wa amani wachukuliwe hatua za sheria ili iwe mfano kwa Watanzania wengine.
  Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewataka Wazanzibari kuyachukua mafunzo ya ibada ya Hijja kuwa mwongozo wa maisha yao ya kila siku.
  Rais Dkt. Shein ameeleza hayo jana wakati alipokuwa akizungumza katika Baraza la Idi Mkoa wa Kusini Unguja.Katika hotuba yake hiyo ambayo alitilia mkazo umuhimu wa wananchi kuishi kwa upendo na kulinda amani na utulivu, aliwaambia wananchi wa Zanzibar kuwa wasichezee amani iliyopo iwe kwa kauli zinazohatarisha amani hiyo ama kwa vitendo.
 "Tusichezee wala tusidharau amani tuliyonayo badala yake tuitunze na tuiendeleze, kwani inapotoweka inachukua muda mrefu na inakuwa vigumu kuirejesha tena hali hiyo," alisema.
  Aliwakumbusha wananchi wa Zanzibar kuwa wao ni watu wamoja hivyo hawana budi kuishi kwa misingi ya udugu, umoja na masikilizano na kusisitiza kuwa bila ya amani Zanzibar haiwezi kufikia malengo iliyojiwekea ya kuendeleza ustawi wa nchi na watu wake.
  Alifafanua kuwa wageni wakiwemo watalii na wawekezaji wanaokuja nchini miongoni mwa vivutio vikubwa kwao ni hali ya utulivu, amani na ukarimu wa watu wa Zanzibar hivyo vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na sifa hizo vinaweza kuathiri uchumi na ustawi wa Zanziba

No comments:

Post a Comment