17 October 2013

TMA YATOA TAHADHARI YA MAFURIKO NCHINI



 Na Penina Malundo
  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imezitaka mamlaka husika kuchukua tahadhari kukabiliana na mafuriko yanayoweza kutokea msimu wa mvua ili kukabiliana na madhara ambayo yanaweza kusababishwa na mafuriko yakiwemo magonjwa ya mlipuko.

 Akizungumza na wadau mbalimbali Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ibrahim Nassib, alisema utabiri unaonesha kutakuwa na mvua za wastani katika baadhi ya maeneo. Nassib alisema TMA inapotoa taarifa za utabiri, mamlaka husika zinatakiwa kushirikiana bega kwa bega ili kujua ni jinsi gani wataepuka madhara yanayoweza kuletwa na mvua hizo.
 Alisema taarifa za mamlaka hiyo zinatakiwa kufanyiwa kazi kikamilifu ili kusaidia wananchi kuepukana na madhara yatakayojitokeza.Aliongeza masuala ya hali ya hewa yanaendana na masuala mbalimbali ikiwemo ya afya, kwani asilimia kubwa mvua za msimu zinapoanza kunyesha hutokea magonjwa mengi ya mlipuko.
  Naye Mjumbe wa Bodi ya TMA, James Ngeleja, alisema taarifa hizo za hali ya hewa ni muhimu kwa masuala ya afya kwani mamlaka hizo zitatakiwa kuchukua tahadhari stahiki ikiwa ni pamoja na kuzibua mitaro na kuondoa mashimo yanayohifadhi mbu.

No comments:

Post a Comment