17 October 2013

DAWA ZA KULEVYA CHANGAMOTO KWA TANZANIA, CHINA-BALOZI



Na Mwandishi Maalum, China
  Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhusiano na China, ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika magereza ya nchini humo, kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya.
Kauli hiyo ilitolewa na Balozi wa Tanzania nchini China , Abdulrahman Shimbo, wakati akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyewasili nchini humo jana kwa ziara ya kikazi.

"Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kimahusiano na China ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya," alisema na kuongeza;
"Kati ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa mashaka. Kati yao 48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10. Kati ya hao 175, wanawake ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China bara."
Akizungumza na maofisa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Waziri Mkuu alisema tatizo la dawa za kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi marafiki.
"Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja, lakini cha kusikitisha zaidi ni idadi kubwa ya wanawake waliokamatwa... wizara zinazohusika inabidi tukae na kuweka mkakati wa pamoja," alisema Pinda.
  Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, Waziri Mkuu alisema, kuna miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake. Aliainisha miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa utalii baina ya Tanzania na China hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja baina ya China na Tanzania.
  Waziri Pinda amewasili Beijing, China saa 10 jana jioni na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.
  Leo Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway Jianchang Engineering

No comments:

Post a Comment