09 October 2013

TAMASHA LA MITINDO REDD'S LAZINDULIWA


Na Fatuma Rashid

   Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's Original, imezindua tamasha la mitindo na ubunifu kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini, litakalojulikana kama 'Redd's Uni-Fashion Bash'
  Akizungumza katika uzinduzi huo Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema tamasha hilo lenye lengo la kuinua vipaji vya wanafunzi katika tasnia ya mitindo, linatarajiwa kuanza mwezi huu na kumalizika mwezi ujao.

Butallah alisema, tamasha hilo kwa sasa litashirikisha vyuo vyote vya elimu ya juu vilivyopo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro na Mwanza.

" Tunataka kuinua vipaji vya wanafunzi wa vyuo katika tasnia ya mitindo, kupitia maonesho yatakayofanywa na wanafunzi wa vyuo hivyo, hapa tunataka wale wenye ubunifu kuonesha ubunifu wao wa mitindo, hivyo hii ni fursa kwao kujitangaza na kudhihirisha uwezo wao," alisema Butallah.

Kuhusu ushiriki, Butallah alisema kutakuwa na fomu maalumu zitakazosambazwa katika vyuo husika, ambapo wanafunzi wanamitindo na wabunifu watazijaza na majaji watazipitia na kupata wabunifu 10 na wanamitindo wa idadi hiyo kutoka kila mkoa, ambao watapata fursa ya kuonesha mavazi yao siku ya tamasha.

  Kuhusu zawadi, Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema kutakuwa na zawadi mbalimbali ambapo washindi watano wa ubunifu na idadi kama hiyo ya wanamitindo kutoka kila mkoa wataondoka na fedha taslimu.

  Edith alisema kwa upande wa wabunifu mshindi wa kwanza ataondoka na sh. 700,000 wa pili sh. 500,000, wa tatu sh. 300,000 huku wa nne na wa tano kila mmoja akiondoka na sh. 100,000. Kwa upande wa wanamitindo mshindi wa kwanza atapata na sh. 500,000 wa pili sh. 400,000 wa tatu sh. 300,000 wakati wa nne na wa tano wakipata sh. 100,000 kila mmoja.

No comments:

Post a Comment