07 October 2013

LISSU APELEKA KILIO KWA JK




  •  ASEMA MEZA YA MAZUNGUMZO ITATOA MWAFAKA
  • ADAI KUSAINI MSWADA NI KUIUNGA MKONO CCM


Rachel Balama na Grace Ndossa
  Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Bw. Tundu Lissu, amesema kama Rais Jakaya Kikwete ana dhamira ya kusikiliza kilio chao kwa njia ya mazungumzo, asisaini Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013 ambao umepitishwa na Bunge, Mjini Dodoma, hivi karibuni
. Bw. Lissu aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mgogoro uliojitokeza bungeni kuhusu mswada huo na suala zima la mchakato wa Katiba Mpya.Alisema kama Rais Kikwete amedhamiria kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani akiamini kilio chao kinazungumzika kwa njia ya mazungumzo ili kufikia mwafaka, asisaini mswada huo.
"Kwa mujibu wa Katiba, Rais ana mamlaka ya kukataa mambo yasiyo na masilahi kwa wananchi na Taifa yanayopitishwa bungeni, ombi letu asisaini mswada huu na kama atafanya hivyo, atakuwa anawaunga mkono wabunge wa chama tawala CCM," alisema.Aliongeza kuwa, mswada huo una kasoro nyingi hivyo ni vyema ukafanyiwa marekebisho kabla hajausaini ili Watanzania waweze kupata Katiba Mpya waitakayo si vinginevyo.
Bw. Lissu alisema ni vyema mazungumzo hayo yakafanyika haraka kwani mchakato wa Katiba ukivurugwa, nchi inaweza kuingia katika machafuko yanayoweza kuzuilika."CCM inataka kuingilia mchakato huo ili kulazimisha mambo ya Muungano ndio maana wanafanya jitihada mbalimbali ili kuuvuruga mchakato huu," alisema Bw. Lissu.
  Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwezi, Rais Kikwete alisema madai ya upinzani yanazungumzika, mengine yangeweza kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha miswada.Alisema kutokuwepo kwao bungeni, hapakuwa na mtu wa kuwasemea ambapo baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.
  "Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa bungeni si vinginevyo, kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko ambayo wanayataka katika sheria hii, naamini na wao wanautambua ukweli huo," alisema Rais Kikwete katika hotuba hiyo.
   Aliwataka viongozi (Wenyeviti) wa vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), waongozwe na hekima kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2012 baada ya kutokea mazingira kama hayo, pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine, kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi.
   Alisema baada ya kuridhiana, hatua zipasazo za kisheria na kanuni, zilichukuliwa na kumaliza mzozo hivyo kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huo zaidi ya kuliingiza Taifa katika matatizo yasiyo ya lazima. Rais Kikwete alisema iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule, inaweza kufanya hivyo hata sasa

No comments:

Post a Comment