16 October 2013

SIMBA SC, YANGA PRESHA INAPANDA, PRESHA INASHUKA


Na Mwandishi Wetu
  Wakati zikiwa zimebaki siku tatu watani wa jadi, Simba na Yanga washuke dimbani wachezaji na mashabiki wa timu hizo mioyo imekuwa ikidunda kutokana na presha ya mchezo huo.

Wakongwe hao wa soka nchini, wanatarajia kushuka uwanjani Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam unaochukua watu 57.
Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 18 wakiwa hawajafungwa mechi hata moja huku watani wao Yanga, wakishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15 wakiwa wamefungwa mechi moja dhidi ya Azam FC.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashabiki wa timu hizo, wanaopenda kukaa makao makuu ya klabu hizo Mtaa wa Msimbazi kwa Simba na Twiga na Jangwani kwa upande wa Yanga, mashabiki hao kila mmoja ametamba timu yake kuibuka na ushindi.
  Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wenzake waliomzunguka katika makao ya Klabu ya Simba, mmoja wa mashabiki hao aliyejitambulisha kwa jina la Chaurembo Ally, alisema ana uhakika na timu yake ya msimu huu tofauti na msimu uliopita.
 "Msimu huu tuna timu nzuri ndiyo maana tuna imani kubwa na mechi hii, tuna washambuliaji wazuri na wenye uchu na pia viungo na mabeki tuna imani nao kubwa hivyo Jumamosi, tunakwenda uwanjani kuongeza pointi tatu muhimu.
  Huku Tamba (Amis), huku Mombeki (Betram) na pale Kiemba (Amri), hapa Chanongo... wamekwisha Yanga, hii si Simba ile waliyoizoea bwana," alitamba shabiki huyo huku akishangiliwa na wenzake.
  Alisema mwaka huu watatangaza ubingwa mapema kutokana na ubora wa kikosi chao kinachotengenezwa na makocha wazawa, Abdallah 'King' Kibadeni ambaye ni Kocha Mkuu akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo 'Julio'.
  Nao mashabiki wa Yanga kwa upande wao, wametamba kwamba Jumamosi hatumwi mtoto sokoni kwa kuwa wana kikosi imara, hivyo Simba wasubiri kipigo.
  Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wenzake, Athuman Libaba alisema licha ya kwamba Simba wanaongoza ligi watahakikisha kipigo cha kwanza wanakumbana nacho Jumamosi.
"Ndugu mwandishi sisi hatuna maneno mengi, sisi kazi yetu ni vitendo tu njoo Jumamosi utaona shughuli yetu, we ukiona manyoya tu ujue kaliwa huyo," alitamba Libaba.

No comments:

Post a Comment