16 October 2013

MADAKTARI WATAKA UFOO SARO AACHWE APUMZIKE



 Leah Daudi na Fatuma Mshamu
  Maendeleo ya afya ya mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro, yameendelea kuwa siri yake na madaktari wanaomtibu hadi siku tatu zijazo ambapo ataruhusiwa kuonana na watu wanaotaka kumjulia hali.Hata hivyo habari zinaeleza kuwa hali ya mwandishi huyo imezidi kuimarika.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaisha, alisema kwa mujibu wa daktari anayemtibu hali yake inaendelea vizuri, lakini hakuna ruhusa ya mtu kwenda kumuona kwani kwa sasa yupo katika mapumziko ya siku tatu.
"Hali yake inaendelea vizuri kutokana na maelezo ya daktari wake anayempatia matibabu, hivyo ni fursa yetu kuweza kumuombea ili aweze kupona," alisema.
Alisema Saro alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili katika wodi ya Kibasila na baadaye kuhamishiwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
  Alisema kuwa kwa sasa, Saro amelazwa katika jengo la matibabu ya moyo na yupo katika wodi za wagonjwa wa kawaida ambapo tangu jana (juzi) hali yake iliendelea kuimarika na jana asubuhi aliweza kuzungumza na daktari wake.
  Wakati huo huo, mwili wa mama yake, Anastazia Peter Saro, umeagwa jana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Ushariki wa Kibwegere Kibamba na kusafirishwa kwenda kijijini kwake Shari, Machame mkoani Moshi kwa mazishi ambayo yatafanyika leo.
  Bi Saro alijeruhiwa Oktoba 13 kwa risasi na mzazi mwenzake, Anter Mushi, ambapo katika tukio hilo alimuua mama mkwe wake (Anastazia) na yeye kujipiga risasi ya kidevuni iliyotokea kichwani na kusababisha kifo chake.Mushi alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Darfur nchini Sudan

No comments:

Post a Comment