16 October 2013

LIGI KUU KUENDELEA TENA LEO Na Fatuma Rashid
  Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inaanza raundi ya tisa leo kwa timu ya Tanzania Prisons kushuka dimbani dhidi ya Ashanti United Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

  Tanzania Prisons ya Mbeya inayofunzwa na Kocha Jumanne Charles inashikilia nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi saba huku Ashanti United ikiwa nafasi ya 13 kwa kuwa na pointi tano.
  Katika mechi ya leo, kila timu itatakiwa kutoka na ushindi ili kujiweka vizuri na kufufua matumaini kwenye msimamo wa ligi hiyo.
  Kikosi cha Prisons, kina wachezaji watatu majeruhi ambao ni Jumanne Elifadhili aliyeumia juu ya jicho na kushonwa nyuzi tatu katika mechi dhidi ya Simba, Jimmy Shoji mwenye kadi tatu za njano na Hamis Maingo aliyeumia bega juzi katika mazoezi.
  Shoji alipata kadi za njano katika mechi dhidi ya Yanga, JKT Ruvu na Simba.Katika mechi iliyochezwa mwishoni mwa wiki, Ashanti iliifunga Coastal Union mabao 2-1 mechi iliyochezwa Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
  Nayo Prisons itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa bao 1-0 na Simba katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam..

No comments:

Post a Comment