16 October 2013

PAC YAZUIA RUZUKU VYAMA VYA SIASA




. David John na Frank Monyo

  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji mstaafu Francis Mutungi, kusitisha utoaji wa ruzuku kwa baadhi ya vyama vya siasa kwa kushindwa kuwasilisha hesabu za ukaguzi wa fedha tangu mwaka 2009.


Agizo hilo lilitolewa Dar es Salam jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe, alipokutana na Msajili huyo ili kufahamu mahesabu ya ruzuku zinazotolewa kwa vyama hivyo.

Bw. Kabwe Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), alisema agizo hilo limeanza jana ili kubaini kama vyama hivyo havikukaguliwa kwa mujibu wa sheria au la.

Alisema uamuzi huo umekuja baada ya Jaji Mutungi kushindwa kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu baada ya kukutana naye kwa lengo la kutaka kujua matumizi ya Fedha hizo ambazo zinatokana na kodi za wananchi.

Alivitaja baadhi ya vyama hivyo kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinapokea sh. bilioni 50.9, CHADEMA sh. bilioni 9.2, CUF sh. bilioni 6.2 na NCCR-Mageuzi sh. milioni 677.

"Hivi ni baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa vikipokea ruzuku, hivyo kamati imemtaka Msajili kwenda kujipanga upya ili atuletee majibu sahihi ya fedha hizo ili kuondoa mgongano uliopo kati ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi ya Msajili," alisema Bw. Kabwe.

Alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 67.7 mwaka 2009 ambazo ni ruzuku kwa vyama vya siasa, lakini tangu mwaka huo hakuna taarifa zozote za mahesabu ya CAG, Ofisi ya Msajili na vyama husika.

"Hizi ni fedha za wananchi ambao ndio wanalipa kodi ambao wanapaswa kujua matumizi ya fedha zao, lazima tupate majibu yaliyokamilika kutoka kwa Msajili," alisisitiza Bw. Kabwe.

  Kutokana na hali hiyo, kamati ilishindwa kuendelea na majadiliano ya matumizi ya fedha za ruzuku hadi ukaguzi huo utakapokamilika ambapo katika kikao hicho, vyama vitatu ndivyo viliitikia wito wa Msajili kukutana na kamati hiyo

No comments:

Post a Comment