16 October 2013

WATU SITA KUNYONGWA HADI KUFA



 Na Suleiman Abeid, Shinyanga

  Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, imewahukumu washtakiwa sita adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwatia hatiani katika makosa ya kuua kwa kukusudia.


Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Simon Lukelelwa aliyekuwa akisikiliza kesi nne tofauti zilizohusu mauaji ya kikatili ambayo yamefanywa kwa wanawake vikongwe kutokana na imani potofu za kishirikina.

Mauaji hayo yalifanyika kati ya 2005 na 2007 katika Wilaya za Shinyanga, Kahama na Bukombe ambako wanawake vikongwe wanne, waliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao hadi kufa.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Venance Nuba na Tegemeo Paulo ambao walitiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Sophia Gundu, Januari 25, 2006, Kijiji cha Kazibizyo, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

  Washtakiwa wengine waliokumbwa na adhabu hiyo ni Joseph Lushika na Maziku Mpigachai waliotiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Monica Bulemela, Mei 6, 2005, katika Kijiji cha Bulembela, wilayani Bukombe.

  Mshtakiwa mwingine ni Mhande Manyanya aliyeshtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mkazi wa Kijiji cha Ihapa, Wilaya ya Shinyanga, Wande Bulugu, Julai mosi 2007,Kijiji cha Ihapa.

  Jaji Lukelelwa pia alitoa hukumu kama hiyo kwa mshtakiwa Tembo Hussein, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimuua kwa kukusudia Anjelina Hungwi, mkazi wa Kijiji cha Itega, wilayani Kahama.

No comments:

Post a Comment