16 October 2013

HAZINA YATUHUMIWA KUHUSIKA NA UFISADI Na Anneth Kagenda
  Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema katika utafiti wake kwenye halmashauri mbalimbali nchini, imebaini kuna mchezo mchafu unaofanywa ambapo vitendo vya ufisadi mkubwa vinaanzia Hazina.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajabu Mohamed Mbaruku aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kwenye ukumbi mdogo wa Bunge ambapo kamati za Bunge zinaendelea.
Alisema, pia vitendo vya ufisadi vinafanywa na watendaji katika Ofisi za mikoa.
Alisema, kabla ya kamati hizo kuanza, kamati yake ilizunguka katika halmashauri na mikoa mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Lindi, Tabora, Morogoro ambapo ilibaini ufisadi huo unafanyika na wanaoufanya ni watendaji ofisi za mikoa na Hazina.
"Kamati yangu ilianza ziara tangu Oktoba Mosi, lakini pia tulibaini ufisadi huo unaofanywa na watendaji wa mikoa na Hazina ambapo wakati mwingine hazina inadai kuwa, fedha zilishapelekwa na ukiziuliza halmashauri zinadai hazijapata fedha hiyo,"alisema Mbaruku.
"Fedha za halmashauri toka hazina haziwafikii, taarifa zinasema zimeenda, lakini ukiuliza wahusika wanadai hazijafika pia tumebaini matatizo mengi ya halmashauri yanafanana, kwani utakuta wameainisha fedha walizopokea, walizotumia, lakini ukiangalia mchanganuo wa matumizi haueleweki,"
"Sasa hatujui kama wanataka kuiongopea kamati au fedha zile wamezichakachua wenyewe... Watendaji katika uvujaji wa fedha za halmashauri kumbukumbu zimekuwa hazioani, mfano utakuta anasema zilizopelekwa ni sh.milioni kadhaa, lakini ukiangalia uhalisia utakuta haviendani,"alisema Mwenyekiti huyo.
  Alisema, katika halmashauri mbili walizokutana nazo jana halmashauri ya Mbulu fedha za Mradi wa Umeme Vijijini (REA) sh. milioni 170 zilipelekwa ambapo sh. milioni 120 zinaonekana zilitumika ila mchanganuo hauoneshi zilitumika vipi na kusema kuwa, hivyo wameidanganya kamati yake na fedha zimeliwa.
  Mwenyekiti huyo pia alisema, wamebaini fedha asilimia 10 za Mfuko wa Wanawake na Vijana ambazo wanatakiwa kuwa wakikopa na kurejesha ambapo halmashauri hutakiwa kuzitoa nazo zimekuwa zikiliwa.
 "Katika mfuko huo wanawake wana asilimia tano na vijana asilimia tano, lakini halmashauri hizo hazipeleki fedha hizo badala yake wanazichakachua pia Halmashauri ya Mbulu tangu kuanzishwa kwa sheria hiyo, miaka mitano iliyopita haijawai kupeleka hata senti tano," alisema. 


   Alisema, kwa mantiki hiyo Mbulu imeamriwa kulipa fedha hiyo mara moja na kusema kuwa katika mfuko huo fedha za serikali zimekuwa zikipelekwa ila halmashauri ndio vikwazo.
  Aidha, alisema baada ya serikali kuondoa kodi kuna asilimia 20 ambayo inatakiwa kwenda vijijini ambapo ilitaka halmashauri kuwa zikipeleka asilimia hiyo, lakini cha kushangaza fedha hizo haziendi ambapo alisema kuwa hali hiyo inaonesha kuwa halmashauri zimeonekana kuwa kidonda ndugu cha kuua maendeleo ya nchi.
  Alisema, katika wiki mbili watakazokuwa kwenye kamati wanatarajia kuzihoji halmashauri 16 na kwamba jana walikuwa na halmashauri ya Babati na Mbulu ambapo pia wamebaini madudu Mbulu.

No comments:

Post a Comment