04 October 2013

NIYONZIMA APATA PIGO  •  MOTO WATEKETEZA NYUMBA YAKE
Na Elizabeth Mayemba

Kiungo wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima amepata pigo kubwa baada ya jana kuunguliwa na nyumba yake iliyopo maeneo ya Magomeni Makuti, Dar es Salaam
.

Kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo, Hafidh Ally ambaye alikuwa katika eneo la tukio alisema moto huo ulisababishwa na shoti ya umeme na kusababisha hasara kubwa kwa mchezaji huyo.

"Kwakweli nipo hapa eneo la tukio baada ya kupata taarifa za mchezaji wetu kuunguliwa na nyumba, tunashukuru Mungu majirani walijitokeza kwa wingi na kusaidia kuuzima moto huo ambao tayari ulikuwa umeshaleta hasara kubwa," alisema Hafidh.

   Alisema moto huo uliibuka sebuleni kwa mchezaji huyo na kuteketeza fenicha zote zilizokuwepo ikiwemo na laptop, lakini thamani halisi ya vitu vilivyoungua haijajulikana kwa kuwa ni vitu vingi vilivyoteketea kwa moto.

   Inadaiwa kuwa, janga hilo lilitokea wakati mchezaji mwenyewe akiwa ndani ya nyumba hiyo na kama si jitihada za majirani kujitokeza kumsaidia kuuzima moto huo, athari ingekuwa kubwa zaidi.

   Imeelezwa kuwa nyumba hiyo ina wapangaji wawili na upande ulioathirika kwa moto ni ambao anaishi mchezaji huyo. Mchezaji huyo amekumbwa na tukio hilo ikiwa ni siku moja tu, tangu adaiwe kuwa anashindwa kuripoti mazoezini kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia yeye pamoja na beki Mbuyu Twite.  

No comments:

Post a Comment