04 October 2013

MAFAO YA WANACHAMA KUFANYIWA UKOKOTOAJI



Na Reuben Kagaruki, Arusha
   Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi na Ajira , Dkt .Makongoro Mahanga, amesema kazi ya kuoanisha kanuni za kukokotoa mafao ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini imefikia pazuri na uamuzi wa mwisho unasubiriwa kutoka ngazi ya juu serikalini.

Mahanga alitoa kauli hiyo juzi mjini hapa wakati akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya washiriki wa mkutano wa 23 wa mwaka wa wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PPF na Wadau Wengine wa Hifadhi ya Jamii mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, kumaliza kuwasilisha mada yake.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alitaka kujua kama SSRA itaweza kuja na kikokotoo kipya cha mafao wakati wanaonufaika na kikokotoo cha sasa ni watendaji wa Serikali ambao ndiyo watoa maamuzi.
“Kikokotoo kibovu wanaonufaika nacho ni wale wale watoa maamuzi waliopo Serikali, sasa hapa dada yangu Irene (Isaka) unadhani utafanikiwa kwa hili? Alihoji Filikunjombe.
Akijibu swali hilo kabla ya Naibu Waziri Mahanga, Isaka alisema hoja ya mbunge huyo ni moja ya changamoto, lakini kazi ya kuoanisha kanuni za kikokotoo cha mafao yote ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii imekamilika na kuwasilishwa Wizara ya Kazi na Ajira.
“Tayari tumekutana na wadau ATE (Chama cha Waajiri) TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania) na Wizara ya Ajira, hatua tuliyofikia ipo ngazi ya juu serikalini,” alisema Isaka na kukiri kuna watu wanaathirika na ukokotoaji wa zamani.
Alisema, wanapoelekea vikokotoo vya mafao wa wanachama wa mifuko ya hifadhi vitafanana ili viendane na kiwango cha michango yao. “Kwa hiyo ninachoweza kusema hapa ni kwamba suala la vikokoto limefika ngazi ya Serikali na Wizara ya imesema suala hilo limefika ngazi ya juu,” alisema Isaka.
   Akikazia jibu la Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Waziri Mahanga alisema; “Suala la vikokotoo SSRA wamemaliza kazi yao na wametuletea sisi wizarani na tumemaliza kazi hiyo, sasa lipo kwenye vikao vya juu vya Serikali, kwa hiyo uamuzi utatolewa wakati wowote ingawa mimi sio ninayehitisha vikao vya Baraza la Mawaziri. Tuwe na matumaini hayo siwezi kusema jambo hili litakwama,” Alisisitiza Mahanga.
   Kuhusu tatizo la mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa chini ya wizara tofauti, Dkt. Mahanga alisema katika nchi nyingi duniani mifuko ya hifadhi ya jamii ipo chini ya wizara moja tena ya ajira.
“Hata sisi hapa kwetu tunaona hili ni jambo zuri, lakini ukiangalia historia iliyoanzisha mifuko hii hauwezi kusema mifuko iwe ndani ya wizara moja,” alisema.
Alisema, suala hilo halina haraka litafanyiwa kazi kama ilivyo maboresho mengine.
“Tunapoelekea ni pazuri tutafikia wakati fulani mifuko yote itakuwa chini ya wizara moja,” alisema Dkt. Mahanga.

No comments:

Post a Comment