09 October 2013

NBC YAZINDUA PROMOSHENI YA 'WEKA UPEWE' NCHININa Mwandishi Wetu
   Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi promosheni ya muda wa miezi mitatu ya kuweka akiba iitwayo 'Weka Upewe' itakayogharimu zaidi ya sh. milioni 300.Promosheni hiyo ina lengo la kuhamasisha wateja wake nchi nzima kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ikiwa ni moja ya matukio ya kuadhimisha Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC
.  Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya benki hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Mwinda Kiula Mfugale alisema kwamba, benki hiyo ipo katika kipindi cha kufurahi na wateja wake, kwa kuonesha umuhimu wao kwa kuwaunga mkono katika kipindi chote cha huduma zao nchi nzima.
 "Kampeni hii si tu ina nia ya kufurahi na wateja wake kwa kuwaunga mkono, lakini pia kuwafanya wateja wawe na utamaduni wa kutunza na kujiwekea akiba kwa manufaa ya baadaye."Tunatarajia kwamba wateja wetu watajitokeza kwa wingi katika kuweka akiba katika Akaunti ya Malengo na Amana Maalum, ambapo watajishindia zawadi mbalimbali kama vile pikipiki, jenereta na gari aina ya Suzuki Swift," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa za Kuwekeza na Wateja Wakubwa, Andrew Masawe alisema kwamba wateja wa benki hiyo kupitia promosheni hiyo wataweza kujifunza kuweka akiba kwa maisha ya baadaye."Kutokana na mazingira ya sasa ya kiuchumi ni muhimu kwa wateja wetu kujifunza namna ya kuweka akiba na matumizi bora ya fedha ikiwemo kuwa na bajeti katika maisha yao ya kila siku," alisema.
  Katika kipindi hiki cha miezi mitatu ya promosheni watapatikana washindi sita ambao watajishindia jenereta, pikipiki na gari. Na ili mteja awe mshiriki ni lazima mteja afungue Akaunti ya Malengo au ya Amana ya Malengo ambayo ni ya mwaka mmoja, lakini pia promosheni hiyo inaweza kuwanufaisha wateja wapya.

No comments:

Post a Comment