09 October 2013

MOAT YATOA TAMKO KUFUNGIWA MAGAZETI Na Godfrey Ismaely

  Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) kimemtaka Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara kuondoa adhabu kwa magazeti yaliyofungiwa yakiwemo Mwananchi, Mtanzania na Mwanahalisi bila masharti
. Wamiliki wa vyombo vya habari nchini walikutana na kujadili suala la Serikali kutoa adhabu za kufungiwa magazeti ambazo zinatolewa mara kwa mara kama yalivyofungiwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa vipindi tofauti kuanzia Septemba 27, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa MOAT, Henry Muhanika ilibainisha kuwa, kikao cha MOAT jana kilikubaliana mambo makuu manne ya msingi."Tuhuma zilizotolewa dhidi ya magazeti yaliyofungiwa zilikuwa za jumla na hivyo hazikukidhi haja ya kuhalalisha adhabu iliyotolewa.

 "Pili kitendo cha kufungiwa magazeti kinaingilia haki ya wananchi kupata habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari kupata ajira," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa, jambo la tatu ambalo wamiliki hao walikubaliana ni kwamba uamuzi wa kuyafungia magazeti unafanywa bila kufuata taratibu na kanuni zinazotakiwa ikiwemo haki ya watuhumiwa kuitwa na kusikilizwa.

  Jambo la nne taarifa hiyo ilibainisha kuwa, kitendo cha kufungiwa magazeti kinapunguza hadhi ya Serikali na kinamchafua rais ndani na nje ya nchi. Aidha, wamiliki wa vyombo vya habari waliishauri Serikali iachane na utaratibu wa kufungia magazeti bali pale inapoona yametokea matatizo itumie mazungumzo na maelewano au ipeleke kesi mahakamani badala ya kuwa mlalamikaji na hakimu.

No comments:

Post a Comment