16 October 2013

TFF YATISHIA KUISHUSHA DARAJA YANGA



 Na Fatuma Rashid
  Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. milioni 5, baada ya baadhi ya viongozi wake kuzuia kituo cha Azam Televisheni kuonesha mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Mtibwa Sugar..

 Mechi hiyo ilichezwa Oktoba 10 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kati ya timu hiyo na Mtibwa Sugar na pia TFF imetishia kuishusha daraja Yanga kama itarudia tena kosa hilo.
  Hii ni mara ya pili katika msimu huu kupigwa faini katika michezo ya Ligi Kuu baada ya awali kutozwa faini ya sh. milioni moja kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu katika mechi dhidi ya Coastal Union, iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na timu zote kutoka sare ya bao 1-1.
  Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema kwa mujibu wa kanuni 32(9) inasema kuwa klabu yoyote itakayozuia chombo chochote cha habari, ambacho kimepewa mamlaka na TFF kuonesha mpira basi faini yake ni sh. milioni 5.
  Angetile alisema kama klabu hiyo itarudia tena kosa, basi adhabu itakayotolewa na TFF ni kushushwa daraja kwa timu hiyo.
  Alisema endapo kama atatokea kiongozi yeyote, atakayezuia mdhamini ambaye pia amepata haki kutoka TFF, kwa mujibu wa kanuni ya 36 kiongozi huyo atafungiwa kutojihusisha na mpira kwa muda wa miaka saba.
  Angetile aliongeza kuwa klabu yoyote haina haki ya kuzuia chombo cha habari kurusha matangazo ya mechi kwani Ligi Kuu ni mali ya TFF

No comments:

Post a Comment