17 October 2013

KUZIONA SIMBA, YANGA ‘BUKU TANO’Na Mwandishi Wetu
  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mechi ya Simba na Yanga Ligi Kuu ya Vodacom itakayopigwa Jumapili Uwanja wa Taifa ambapo cha chini kitakuwa sh. 5,000.Kiingilio cha sh. 5,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.

  Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tiketi moja itapatikana kwa sh. 30,000.
 “Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni katika vituo mbalimbali.“Vituo hivyo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/ Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani,” alisema Wambura.
  Wambura alisema mechi hiyo namba 63 itachezeshwa na Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam, ambapo atasaidiwa na Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam pia na Ferdinand Chacha wa Bukoba. Mwamuzi wa akiba ni Oden Mbaga wa Dar es Salaam.
  Alisema Kamishna wa mechi hiyo atakuwa, John Kiteve kutoka Iringa wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Stanley Lugenge wa Njombe.
  Wakati huo huo, Wambura alisema mechi tatu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) katika kundi A na C, zimesogezwa mbele kutokana na viwanja vya Kambarage, Shinyanga na Nangwanda Sijaona, Mtwara kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
  Alisema katika kundi A, mechi kati ya Ndanda na Transit Camp iliyokuwa ichezwe Oktoba 19 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
  Ofisa huyo alisema Stand United na JKT Kanembwa zilizokuwa zicheze Oktoba 19 mwaka huu, sasa mechi hiyo ya kundi C itafanyika Novemba 2, mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Nayo mechi ya Mwadui na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo Oktoba 26, mwaka huu imesogezwa hadi Novemba 3, mwaka huu.
 

No comments:

Post a Comment