01 October 2013

KUFUNGWA MAGAZETI: HOJA BINAFSI KUTUA BUNGE  • MCT,CHADEMA,NCCR, TAASISI ZATOA TAMKO  

   Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), ametoa taarifa kwa katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za Bunge kuelezea kusudio lake la kuwasilisha mswada binafsi wa marekebisho sheria ya magazeti ili ifutwe kabisa, anaripoti Anneth Kagenda na Darlin Said.

   Taarifa aliyoitoa Dar es Salaam jana kwenye vyombo vya habari, ilisema lengo la kushawishi kufutwa kwa sheria hiyo ya mwaka 1976 ni kwa sababu inakinzana na Katiba ya Nchi juu ya haki za raia kupata habari.Alisema mswada huo atauwasilisha Ijumaa ili uchapwe katika gazeti la Serikali uweze kuingia kwenye shughuli za Bunge ambazo zitaanza Oktoba 15 mwaka huu, ngazi ya kamati.
   Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, amemshauri Bw. Kabwe auwasilishe mswada huo kama wa haraka kwani ukienda kwa taratibu za kawaida, kuna vikwazo vya kikanuni, kiserikali na kibunge.Alisema vikwazo hivyo vitatumika kuukwamisha kwa kuzingatia wakati suala hilo limelenga kuyanusuru magazeti yasiendelee kufungiwa hivyo hatua za haraka zinahitajika.
   Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa kanuni za bunge, mswada wa mbunge binafsi ukipelekwa, kawaida serikali ndiyo yenye kazi ya kuuchapa katika gazeti la serikali kabla ya kwenda Kamati za Bunge na bungeni hivyo unaweza kukwamishwa.
   Katika hatua nyingine, Baraza la Habari nchini (MCT) limelaani uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti hayo yakidaiwa kuchapisha habari za uchochezi na kujenga chuki ili kuushawishi umma ukose imani na vyombo vya serikali.
  Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, ilisema hatua zilizochukuliwa na serikali si za kidemokrasia na zimeirudisha nchi miongo 10 nyuma katika jitihada zake za kujenga jamii ya kidemokrasia ambayo inaheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.
  “Uhuru wa kujieleza ni muhimu zaidi kuliko haki zote, nchi inayodai kufuata kanuni za kidemokrasia na maadili ya haki za kibinadamu kama Tanzania inapaswa kulinda haki hii ya msingi.“Serikali inapaswa kutafuta njia nyingine za kurekebisha matukio ambayo wanadhani ni uwakilishaji mbaya wa kazi zake unaofanywa na vyombo vya habari pamoja na kufanya mazungumzo,” alisema.
  Baraza hilo limewataka wadau wa vyombo vya habari na umma kwa ujumla kuunga mkono juhudi zake za kukazania kufutwa kwa sheria mbaya zinazokandamiza uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari pamoja na upatikanaji habari.
  Wakati huo huo, wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu na wadau mbalimbali, wametoa tamko la kupinga kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania na kuiomba Serikali iyafungulie mara moja.
  Tamko hilo lilisomwa na Mratibu wa Mtandao huo (THRD-Coalition), Onesmo Olengurumwa, kwa niaba ya wenzake mbele ya waandishi wa habari na viongozi mbalimbali wa mitandao hiyo zaidi ya 50.
  Alisema ni vyema Serikali ikatumia njia shirikishi kama mahakama na Baraza la Habari nchini (MCT) kupeleka malalamiko yake badala ya kuvifungia vyombo hivyo.“Serikali izifute na kuzifanyia marekebisho sheria zote kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, kufungiwa kwa vyombo hivi kunaleta hofu kwenye jamii,” alisema.
   Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara na Taasisi za Dola na Vyombo vya Uwakilishi wa Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. Faustine Sungura, alisema wamesikitishwa na kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti hayo wakati wananchi wanahitaji taarifa hasa kipindi hiki cha katiba.
   Alisema Serikali imeamua kuyafungia magazeti hayo bila kuwatangazia wananchi nani mlalamikaji wa mwenendo mbaya wa magazeti hayo kama ilivyodai serikali.

No comments:

Post a Comment