01 October 2013

KUTEKWA KWA DKT. ULIMBOKA:MSHTAKIWA HURU KWA FAINI 1,000/-



  •  NI MKENYA ALIYEDAIWA KUMTEKA,KUMTESA
  • ASIMULIA MKASA,MWANDISHI AMLIPIA FAINI

Na Rehema Mohamed
 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemlipisha faini ya sh. 1,000 raia wa Kenya, Bw. Joshua Mulundi baada ya kumtia hatiani katika kesi iliyokuwa ikimkabiliBw. Mulundi alikuwa akikabiliwa na kesi ya kuidanganya polisi kuwa alihusika katika tukio la kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka.

 Shauri hilo lililetwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Aloyce Katemana, kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali na upande wa mashtaka ambapo Bw. Mulundi, alikiri kutenda kosa hilo.Hakimu Katemana aliieleza Mahakama hiyo kuwa, baada ya mshtakiwa kukiri maelezo yote ya kosa, inamtia hatiani na kumsomea hukumu pamoja na adhabu ya kulipa sh. 1,000 au kifungo cha miezi sita gerezani.
 Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Katemana alisema hukumu hiyo imezingatia maelezo ya upande wa mashtaka na mshtakiwa alipokuwa akiililia mahakama, hivyo kumpa adhabu ya kulipa faini au kwenda gerezani miezi sita.
 Hata hivyo, Hakimu Katemana alipomuuliza mshtakiwa kama ana kiasi hicho cha fedha alijibu hana ambapo mwandishi wa habari wa Kituo cha Radio Times FM, Chipangula Nandule alijitolea kumlipia faini hiyo.Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Bw. Mulundi alidai mahakamani hapo kuwa, alikuja Tanzania kufanya biashara ya nguo ambayo aliunganishwa na kijana mmoja wa mjini Arusha ambapo akiwa huko, Juni 27, 2012 alitekwa na mtu asiyemjua.
 Alisema mtu huyo alikuwa na silaha, kumpeleka asikokujua na kumlazimisha aende kwenye Kanisa la Ufufufo na Uzima la Mchungaji Gwajima lililopo Kawe, Dar es Salaam akasema alichomueleza ambacho ni kumteka Dkt. Ulimboka. Alidai alilazimika kukubaliana na amri hiyo kutokana na vitisho alivyokuwa akipewa na baada ya hapo, alipelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay na kusisitizwa azungumze alichokisema na kuahidiwa atapelekwa kwao nchini Kenya na kubadilishiwa maisha yake.
 Huku akibugujikwa na machozi, Bw. Mulundi alidai “Nikiwa Polisi Central, polisi mkubwa aliniambia niseme vilevile nilivyoambiwa niseme na walinirekodi, nilishangaa kuletwa mahakamani nikidaiwa kutaka kumuua Dkt. Ulimboka.
 “Sipingani na upande wa mashtaka, nilivyoletwa nilidhani nimeonewa, nimejifunza kuwa mahakama ni kitu tofauti sana, siilaumu Serikali, polisi wala upande wa mashtaka maana hata nisingekubaliana na walioniteka, mimi si bora zaidi ya watu wengine,” aliongeza mshtakiwa huyo.Alisema kuwa, tukio la kutekwa Dkt. Ulimboka lilileta shida nchini lakini taarifa alitoa kwa hiari yake kutokana na vitisho alivyokuwa akivipata ili kuokoa maisha yake.
  “Mheshimiwa hakimu, nimekosa mbele ya Mungu na mahakama ya Tanzania, ningeomba kwa ubinadamu na upendo pia, nimekaa jela muda mrefu, naomba nipewe adhabu iwe fundisho kwa wengine lakini nipunguziwe adhabu,” alidai.Bw. Mulundi alidai yeye ni kijana wa miaka 23, mama yake ni mjane hivyo yupo mwenyewe nyumbani kwao hivyo hakimu akiwa kama mazazi, amuonee huruma kwani hajui kitakachofanyika kesho.
  Awali akisomewa maelezo hayo ya awali na wakili wa Serikali Tumaini Kweka, alidai mshtakiwa huyo alikuja nchini akipitia mpaka wa Namanga, Arusha-Dar es Salaam na kwenda kanisani hapo.Alidai mshtakiwa huyo alionana na Mchungaji Joseph Kiriba na kumweleza kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliomteka na kumtesa Dkt. Ulimboka, kumtupa Mabwepande na taarifa kufika polisi.
  Aliongeza kuwa, baadaye mshtakiwa huyo alipelekwa kwa mlinzi wa amani ambapo alikanusha taarifa za kumteka Dkt. Ulimboka. 
  Alidai baada ya polisi kufanyia uchunguzi taarifa hizo, ilibaini ni kweli hakuhusika hivyo kumbadilishia mashtaka kutoka lile la kumteka na kumjeruhi, Dkt Ulimboka hadi shtaka la kutoa taarifa za uongo kwa polisi na kushtakiwa upya

No comments:

Post a Comment