17 October 2013

HOSPITALI YA UPASUAJI WA MOYO KUJENGWA NCHINI Na Rachel Balama
  Hospitali ya Kimataifa ya upasuaji wa moyo inatarajiwa kujengwa nchini na Hospitali ya PARAS iliyopo nchini India baada ya kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji yaliyopo nchini Tanzania.

Hayo yalisemwa na mbunge wa zamani wa Njombe kwa tiketi ya CCM, Yono Stanley Kevela, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mara baada ya ziara yake ya mwezi mmoja nchini India kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wawekezaji kuja nchini.
Kevela alisema Watanzania wengi wanalazimika kwenda nchini India kutibiwa maradhi mbalimbali kutokana na utaalamu huo kukosekana nchini, hivyo ujio wa hospitali hiyo utakuwa fursa ya kipekee.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusafiri kwenda nchini, India kwa matibabu hayo.
  Alisema gharama za matibabu nchini India ni rahisi ila kinachowakwamisha Watanzania wengi kwenda ni usafiri na gharama za kuishi nchini humo.
  Kevela ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Yono Auction Mart, alimtaja Dkt. Kapil Gargi ambaye ni mratibu wa kanda wa hospitali ya PARAS kwamba ndiye atakuwa mratibu wa mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo.
"Tuna tatizo la watu kutokupima afya zao, mfano unaweza kumpeleka mgonjwa India kwa matibabu lakini wewe unayemsindikiza mgonjwa ukipimwa unakutwa ndiye mgonjwa zaidi ya yule uliyempeleka," alisema Kevela.
  Aliongeza kuwa licha ya maji kuwa na umuhimu mkubwa katika ujenzi wa mwili imara, lakini watu wengi hawana utamaduni wa kunywa maji mengi hadi pale wanaposhauriwa na madaktari.
 Kevela alisema amezungumza na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi ambapo ameonyesha kufurahia mpango huo na kuwataka Watanzania wengine kuiga mfano wa Kevela kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini.
  Pia alisifu jitihada za Balozi wa Tanzania nchini India, Injinia John Kijazi za kuhamasisha wawekezaji nchini India kuja kuwekeza hapa nchini na kwamba hata PARAS imevutiwa kuja kuwekeza kutokana na jitihada za balozi huyo.

No comments:

Post a Comment