21 October 2013

CUF YAMTEGA ZITTO KABWE



  •  WAIPINGA PAC,WAJIPANGA KUCHUKUA HATUA
  • WATISHA KUSUSIA KIKAO CHAKE OKTOBA 25

Rachel Balama na Anneth Kagenda
  Chama cha Wananchi (CUF), kinatafakari hatua za kuchukua pamoja na kumuandikia barua Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda aweze kuzifunda Kamati za Bunge ili zitambue wajibu wake.Tamko la CUF linatokana na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Zitto Kabwe, kuvitangazia kiama vyama tisa vya siasa vinavyopata ruzuku lakini vimeshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha.

Taarifa za ukaguzi huo zilipaswa kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa (CUF) Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema chama hicho kinatekeleza sheria zinazovitaka vyama vya siasa kupeleka hesabu zao ili zikaguliwe na vyombo maalumu vya Serikali.
Alisema chama hicho hakihusiki na agizo la Bw. Kabwe aliyedai chama hicho ni miongoni mwa vyama vinavyopewa ruzuku na kimeshindwa kuwasirisha taarifa za ukaguzi wa fedha kwa CAG katika kipindi cha miaka minne.
 "Pamoja na kumwandikia Spika barua, CUF haitakutana na Kamati ya PAC, Oktoba 25 mwaka huu kama alivyodai Bw. Kabwe kwa sababu hatujapewa barua ya wito hivyo hatuwezi kuitwa kihuni kupitia mitandao ya kijamii.
 "Hiki ni chama cha siasa ambacho kina utaratibu wake, hatuwezi kuitwa katika mkutano kupitia facebook, twiter, whasapp, google na mitandao mingine ya kijamii, Oktoba 25 hatuendi na gerezani hatuwezi kupelekwa... vielelezo vyote tunavyo na tayari vimehakikiwa na Msajili wa Vyama," alisema.
  Aliongeza kuwa, PAC imeamua kuligeuza jambo hilo kuwa mtaji wa kisiasa na kusisitiza kuwa, hesabu ambazo chama hicho hakijawasilisha kwa CAG ni zinazoishia Desemba 31,2012 ambazo wakaguzi wa ndani na nje wamemaliza kuzikagua Julai mwaka huu.
Bw. Mtatiro alisema, hesabu hizo zitathibitishwa na Kikao cha Kamati ya Utendaji Taifa mwezi huu na Baraza Kuu la Uongozi Desemba mwaka huu hivyo hesabu ambazo bado hazijamfikia Msajili ni za mwaka mmoja uliopita.
  "Tumesikitishwa na kauli tulizozisikia kupitia vyombo vya habari kuwa CUF ni miongoni mwa vyama vilivyoshindwa kuwasilisha hesabu zake kwa CAG miaka minne mfululizo, tunaomba Watanzania wazipuuze taarifa hizo kwa sababu hazina ukweli wowote," alisema Bw. Mtatiro.
  Alisema Bw. Kabwe hana taarifa za kina jinsi CUF ilivyotekeleza wajibu wake na kama Kamati ya Bunge inafanya kazi zake katika mitandao ya kijamii ni jambo la kufedhehesha."Kamati makini ya Bunge ni ile inayopokea taarifa kutoka pande zote muhimu, inakutana na wadau wote, kujua tatizo liko wapi na kuujulisha umma nani amesababisha uzembe," alisema. Hivi karibuni Bw. Zitto alivishutumu vyama vyote vinavyopokea ruzuku na kudai vimeshindwa kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa hesabu kwa CAG na Msajili wa Vyama vya Siasa.

2 comments:

  1. Hongera Mtatiro kwa ufafanuzi mzuri umeonesha CUF mko safi kiasi gani. Endeleeni na utamaduni huo kwani nchi hii nyinyi ndio tegemeo letu baada ya ccm mafisadi.

    ReplyDelete