21 October 2013

JULIUS NYAISANGA AFARIKI DUNIA



Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
  Mtangazaji mkongwe na aliyekuwa Meneja wa Kituo cha Abood Media, mkoani Morogoro, Julius Nyaisanga kwa jina maarufu (Uncle J), amefariki dunia jana saa moja asubuhi katika Hospitali ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro
.Akizungumza na Majira, Meneja Matangazo wa kituo hicho, Bw. Abed Dogoli, alisema marehemu Nyaisanga alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari. Alisema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Kihonda na atasafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.
Mke wa marehemu, Bi. Leah Nyaisanga alisema mumwe alizidiwa juzi jioni na kupelekwa hospitalini hapo ambapo kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yao, wadau wa tasnia ya habari na Watanzania kwa ujumla.
"Marehemu aliwahi kufanya kazi kwenye Kampuni ya IPP, akiwa Mkurugenzi wa Radio One, awali aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania wakati huo ikiitwa (RTD)," alisema..Mbunge wa Morogoro Mjini, Bw. Aziz Abood (CCM), alisema amepokea taarifa za msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwani marehemu alijituma na kufanya kazi zake vizuri.
"Nilimfahamu marehemu miaka mingi tangu akiwa kwenye vituo mbalimbali vya utangazaji na alikuwa mahiri," alisema..Marehemu Nyaisanga ameacha mke na watoto watatu ambao ni Samuel, Noela na Beatrice. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi

No comments:

Post a Comment