Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga
JESHI la Polisi mkoani Rukwa limemkamata na kumfikisha mahakamani aliyekuwa diwani wa viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sumbawanga, Bora
Mohamed (40) kwa tuhuma za kupatikana na Kompyuta ya wizi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage diwani huyo mkazi wa Kitongoji cha Majengo Manispaa ya Sumbawanga alikamatwa juzi saa 9:30 mchana akiwa katika kituo cha daladala ya Chanji akiwa na seti moja ya
kompyuta yenye thamani ya sh. 400,000 akiwa katika harakati za kuiuza.
Akifafanua zaidi juu ya tukio hilo, Kamanda Mantage alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa akienda kuiuza katika Kitongoji cha Kizwite kilichopo ndani ya manispaa hiyo.
Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, diwani huyo alisema kuwa
mali hiyo ni ya kwake lakini baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi, kompyuta hiyo ilitambuliwa kuwa iliibwa kwa Mwalimu Mjwadu Babala wa Shule ya sekondari Mafulala baada ya nyumba yake iliyopo eneo la Bangwe kuvunjwa na watu wasiofahamika na kuiba vitu mbalimbali January 26, mwaka huu.
Hata hivyo, Kamanda Mantage alisema kuwa katika tukio hilo mwalimu huyo alilipoti kuibiwa kwa vitu mbalimbali ikiwemo pikipiki pamoja na kompyuta baada ya kuipekua walibaini kuwepo kwa nyaraka mbalimbali zilizomhusu mwalimu huyo.
Mtuhumiwa huyo tayari amekwisha fikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo za wizi.
No comments:
Post a Comment