18 September 2013

YANGA SC VITANI TENA LEO SOKOINE

Na Hamisi Miraji, Mbeya

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo jioni watajitupa uwanjani kumenyana na Prisons, mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Sokoine.Mchezo huo utakuwa wa aina yake ikizingatiwa kuwa Yanga, ipo katika wakati mgumu kutokana na mchezo wao dhidi ya Mbeya City kufanyiwa vurugu na mashabiki, jambo lililosababisha basi lao kuvunjwa kioo
. Mbali ya kuwa na hofu na mchezo huo, Yanga inapokutana na Prisons katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya huwa wanapata tabu kutokana na uwanja wake kutokuwa na kiwango kizuri.Timu zote zitaingia uwanjani zikiwa na uchu wa kushinda, kwani katika michezo yao ya Jumamosi, Yanga walitoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City huku Prisons ikitoka suluhu dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Msimu uliopita timu hizo katika mzunguko wa kwanza zilitoka suluhu katika Uwanja wa Sokoine na mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi.Katika mchezo wa leo, Polisi jijini Mbeya watalazimika kuweka ulinzi mkali kutokana na vurugu za mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, ambapo mashabiki waliwashambulia Yanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya amewataka Yanga, kutoingia uwanjani na hofu ya vurugu na kuwahakikishia kile kilichotokea Jumamosi hakitojirudia.Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts akizungumzia mchezo wa leo kwao, alisema unaweza kuwa mgumu kwani wachezaji wake wameathirika kisaikolojia kutokana na mashabiki wa Mbeya kuwanyima raha.

Hata hivyo alisema, timu yake imejiandaa vya kutosha kuukabili mchezo huo kwani wachezaji wake wote wako vizuri, anaamini watashinda na kujizolea pointi tatu muhimu."Mchezo utakuwa mgumu, lakini tumejiandaa vizuri pamoja na kuuzoea uwanja kama kutakuwa hakuna vurugu naamini tutashinda," alisema.

Naye Kocha wa Prisons, Jumanne Chale alisema hawana wasiwasi na Yanga kwani kikosi chake kipo vizuri na ikizingatiwa wanacheza katika uwanja wa nyumbani, ingawa kwenye mchezo lolote linaweza kutokea.

Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' alisema watazimalizia hasira zao katika mchezo wa leo kutokana na kitendo walichofanyiwa Jumamosi dhidi ya Mbeya City.Wakati Yanga wakiwa jijini Mbeya, watani wao wa jadi Simba wao watakuwa jijini Dar es Salaam kuwakaribisha maafande wa Mgambo JKT, huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kutoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja huo.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar, wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.

No comments:

Post a Comment