- HATIMA YA WALIOPANDA FEDHA SAS NJIA PANDA
- DPP AKATA RUFAA,APINGA AMRI YA MAHAKAMA
Na Rachel Balama
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha kusudio la kukata
rufaa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam dhidi ya vigogo wa Kampuni ya
Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI).
Kampuni hiyo ilikuwa ikiendesha na
kusimamia mchezo wa upatu ambapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa,
iliwasilishwa katika mahakama hiyo Agosti 23 mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, katika kusudio
hilo DPP anapinga amri iliyotolewa na mahakama
hiyo kuitaka Serikali pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ifanye utaratibu wa
kurudisha fedha zilizopandwa na wanachama wa kampuni hiyo.
Wanachama hao ni wale watakaoonesha
uthibitisho wa kupanda fedha zao DECI ambapo DPP anataka mahakama itamke wazi
na kutoa maelekezi ni nani anayestahili kurejesha fedha hizo kwa wanachama hao.
Katika hukumu iliyotolewa na mahakama
hiyo Agosti 19 mwaka huu, mahakama iliwahukumu vigogo wanne kati ya watano
kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. milioni 21 kila mmoja.
Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Aloyce
Katemana kwa niaba ya Hakimu Stuwart Sanga aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na
kudai kuwa, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa
yakiwakabili washtakiwa na kuwatia hatiani.
Hakimu Katemana alisema, pamoja na
hukumu hiyo Serikali ifanye mchanganuo wa mali
za DECI ambazo inazishikilia kwa kuwa zipo mali ambazo zinashikiliwa lakini ni
za watu wengine.
Washtakiwa waliotiwa hatiani katika
kesi hiyo ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Ole Loitignye na Samwel
Sifael Mtares ambapo mshtakiwa Arbogast Kapilimba aliachiwa huru baada ya
mahakama kushindwa kumtia hatiani.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao
wanakabiliwa na
mashtaka mawili ambayo ni kuendesha na
kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya
Adhabu Sura ya 16.
Ilidaiwa kuwa, kati ya mwaka 2007 na
Machi 2009, katika Makao Makuu ya DECI, yaliyopo Mabibo Mwisho, Dar es Salaam, washtakiwa
waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini kwa ahadi
ya kuwapa wanachama wake fedha zaidi.
Shtaka la pili ni kupokea amana za umma
bila kuwa na leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na
Taasisi za Fedha namba 5 ya mwaka 2006 na kwamba washtakiwa wote katika kipindi
hicho, wakiwa kwenye Ofisi za DECI, walipokea amana kutoka kwa umma bila leseni.
DECI iliwanufaisha watu wengi hasa
waliojiunga mwanzoni na badaye kuibuka malumbano kati yao, Serikali na wanachama waliopinga
kusitishwa kwa shughuli za taasisi hiyo.
Kusimamishwa kwa shughuli za DECI,
kulitokana na uamuzi wa BoT kutoa taarifa ya kuwahadharisha Watanzania
waliojiunga na upatu huo kuwa taasisi hiyo haiko kisheria na wanaweza kupoteza
fedha walizopanda.
Upandaji mbegu katika taasisi hiyo,
ulisitishwa baada ya Serikali kusimamisha akaunti za taasisi hiyo hadi
uchunguzi utakapokamilika na kusababisha uvunjifu wa amani kwa wanachama wa
DECI na viongozi wa taasisi hiyo.
Baadhi ya wanachama waliamua kuchukua
sheria mkononi kwa kuvunja vioo vya magari ya viongozi, wakitaka warejeshwe
fedha zao.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri
ulikuwa unawakilishwa na Wakili, Prosper Mwangamila na Justus Mulokozi, ambapo
washtakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo
na Onesmo Kyauke.
Wakili wa DECI
Siku moja baada ya mahakama hiyo kutoa
hukumu, Majira lilizungumza na Wakili wa washtakiwa Bw. Ndusyepo, ambaye
alisema kuwa, mahakama hiyo imeshindwa kusimamia vizuri sheria iliyowatia
hatiani wateja wake na kuwaacha wanachama.
Alisema yeye hapingani na hukumu
iliyotolewa na mahakama lakini sheria ya adhabu kifungu cha 171 (A), kama ilivyorekebishwa na sheria namba 8 ya mwaka 2006,
haikutekelezwa ipasavyo.
Bw. Ndusyepo alisema sheria hiyo pia
inawatia hatiani wanachama wote waliopanda fedha zao DECI kwa kushiriki upatu,
hivyo mahakama inapotoa amri kwa Serikali irudishe fedha za wanachama hao ni
sawa na kuwazawadia wahalifu.
Aliongeza kuwa, kama
sheria hiyo imetumika kuwatia hatiani wateja wake, haikupaswa kuwaacha
wanachama ambao kwa mujibu wa sheria nao walipaswa kutiwa hatiani kwani kitendo
cha kushiriki upatu kinakatazwa na sheria hiyo.
“Wanachama wa DECI nao ni wahalifu kwa
mujibu wa sheria hii hivyo walipaswa kutiwa hatiani kwa kujihusisha na upatu
ambao upo kinyume cha sheria.
“Haikuwa rahisi kuwakusanya wanachama
wote na kuwaunganisha katika hati ya mashtaka moja ndio maana ilikuwa rahisi
kuwashtaki Wakurugenzi kwa niaba ya wote,” alisema.
Aliongeza kuwa, amri iliyotolewa na mahakama hiyo kutaka wanachama
wa DECI warudishiwe fedha zao inaondoa dhana ya Bunge kutunga sheria inayozuia
mchezo wa upatu.
No comments:
Post a Comment