24 September 2013

WAZIRI MGIMWA: KIPATO CHA MTANZANIA KIMEONGEZEKA



 Leah Daudi na Penina Malundo
   Pato la taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka 2012 kutoka asilimia 6.4 mwaka 2011.Aidha, pato la mtu binafsi limekuwa kwa asilimia 75 sawa na sh. 770,464 kwa mwaka.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya majukumu ya wizara yake
.  Dkt. Mgimwa alisema kuwa, katika robo ya kwanza inayoishia mwezi Machi 2013 pato limekua kwa asilimia 7.5, kwa mwaka huu.
“Wizara imefanikiwa kutathmini hali ya umaskini nchini na kubaini kuwa pato la kila Mtanzania limeendelea kukua na kufikia wastani kwa kila mtu sh.1,025,038 kwa mwaka 2012 kutoka sh. 770,464.3 kwa mwaka 2010,”alisema Dkt. Mgimwa.
Alisema kuwa, lengo la Serikali ni kudhibiti kasi ya vitu kupanda bei ili kuwa katika kiwango cha tarakimu moja ambayo kwa mwaka 2011, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 19.8 na kushuka hadi 6.7,hivyo Wizara yake inatarajia kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kunakuwepo chakula cha kutosha nchini.
Alisema kuwa, asilimia 75 ya wananchi vijijini hawaguswi na uchumi wa nchi, hivyo bajeti ya sasa inapunguza kodi ya uingizwaji wa vifaa vya umwagiliaji,
Sambamba na kuhakikisha kufikiwa kwa pembejeo kwa wakati pamoja na usafirishaji wa mazao yao kwenda katika masoko kwa urahisi kwa lengo la kukuza hali ya mapato vijijini.“Wizara ya Fedha tunafanya kazi ili kukuza mapato yao,” alisema.
  Alisema kuwa, kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa bajeti ya mwaka wa fedha kutoka Juni kwenda Aprili, utaweza kuhakikisha ofisi mbalimbali za Serikali ambazo zinasimamia mapato ya serikali kufanya haraka kutoa ripoti ya fedha ili fedha ziweze kuharakishwa katika wizara zake.
  Wakati huo huo, Dkt. Mgimwa alisema kuwa, kwa sasa serikali inatoza dola 152 kwa magari yanayoingia kutoka nchi ya Rwanda kama serikali ya Rwanda inavyo toza magari ya Tanzania.  

No comments:

Post a Comment