24 September 2013

ICC YAMPA RUTO RUHUSA KURUDI KENYA



THE HAGUE, Uholanzi
    Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wameahirisha kesi inayomkabili Makamu wa Rais nchini Kenya, Bw. William Ruto kwa wiki moja.Bw. Ruto na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo, wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu wakidaiwa kuhusika na ghasia za kikabila baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2007-2008 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa.

   Uamuzi huo umelenga kumpa Bw. Ruto nafasi ya kurejea nchini kwake ili kuangalia hali ya kiusalama baada ya kundi la wanamgambo wa Al Shabaab, kuliteka jengo la ghorofa nne lenye maduka la Westgate, jijini Nairobi.
   Tukio hilo limetokea Septemba 21 mwaka huu, ambapo hadi jana, idadi ya watu walioripotiwa kufa ni 69, majeruhi 175 na mateka wengine bado wameendelea kuzuiliwa. Mahakama hiyo iliahirisha kesi baada ya kikao cha dharura kuitishwa ambapo upande wa mashtaka ulisema hauna pingamizi lolote kama kesi hiyo itaahirishwa kwa muda mfupi.
   Mwakilishi wa mashahidi wa kesi hiyo aliangua kilio mahakamani na kutaka mahakama iweze kumruhusu Bw. Ruto arejee nyumbani kushughulikia suala hilo la dharura.“’Kutokana na hali ilivyo na maoni tuliyoyasikia, mahakama inamruhusu Bw. Ruto kurejea nyumbani kwa muda wa wiki moja,’” alisema Jaji anayesimamia kesi hiyo, Chile Eboe-Osuji.
     Kwa mujibu wa wakili Karim Khan, anayemtetea Bw. Ruto, alisema mteja wake alitarajiwa kuondoka Uholanzi jana saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki kurudi Kenya

No comments:

Post a Comment